![]() |
| Msongamano katikati ya jiji la Dar es Salaam kama unavyoonekana pichani. |
Mvua iliyonyesha jijini Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti, kwa kiasi kikubwa imesababisha foleni ya magari katika maeneo mengi na kuleta usumbufu kwa watumiaji wa barabara hususani wenye magari.
Hata hivyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa kupitia kwa Mkurugenzi wake, Dk Agness Kijazi, imesema mvua hiyo inayotarajiwa kuendelea kunyesha tena leo na kesho, haina madhara makubwa kama miundombinu ipo katika hali nzuri.
Mvua hiyo iliyoanza kunyesha saa tatu za asubuhi na kukatika katika, ilisababisha foleni ya magari hasa katika maeneo ya Posta, Kariakoo, Magomeni, Akiba, Fire na kwingineko huku gazeti hili likishuhudia magari yakikaa katika eneo moja kwa zaidi ya dakika 45.
Barabara ya Samora, Ali Hassan Mwinyi, Mandela, Kilwa, Nyerere, Kawawa na Uhuru, kulikuwa na foleni kubwa huku askari kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani wakijaribu kuondoa usumbufu uliokuwa ukijitokeza katika baadhi ya maeneo.
Aidha, baadhi ya nyumba zilizopo kando kando ya mradi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi (DART) kuanzia eneo la Manzese hadi Jangwani, zilishuhudiwa zikiingiwa na maji kutokana na barabara hizo kufurika maji yaliyotokana na mvua hiyo.
Kijazi alisema mvua hiyo ni matokeo ya mkusanyiko wa upepo katika pwani ya Mashariki, hivyo haitarajiwi kunyesha kwa kipindi kirefu na kuongeza kuwa Mamlaka itaendelea kutoa taarifa kwa kipindi chote kadri hali itakavyokuwa ikibadilika.
“Ni mvua ya kawaida haionyeshi kuwa na madhara sana kulingana na uchunguzi wetu, isipokuwa madhara yanaweza kujitokeza katika maeneo yenye miundombinu mibovu , pia kuziba kwa mitaro ya maji katika maeneo hayo kunaweza kuleta madhara” alisema Kijazi.
Aidha, aliwataka wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari ikibidi kuyahama maeneo hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza mara mvua rasmi zitakapoanza wakati wowote katikati au mwishoni mwa mwezi huu.

No comments:
Post a Comment