Friday, October 11, 2013

MGOMO WA MALORI WAKWAMISHA MELI 15 ZA MAGARI BANDARINI DAR...

Meli bandarini Dar es Salaam.
Mgomo wa malori uliokwisha jana, umeathiri shughuli za Bandari ya Dar es Salaam, ambayo imejikuta imezidiwa na shehena ya mizigo.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Janeth Ruzangi, alisema hayo jana alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuzungumzia utendaji kazi wa Boya la Mafuta la SPM Kigamboni.
Kwa sasa bandari imesheheni tani 23, 165 za mbolea zilizokwama bandarini hapo kutokana na mgomo huo.
“Mbolea nyingi iliyopo bandarini sehemu kubwa inaenda Zambia na nyingine ni ya matumizi ya hapa nchini... meli zikifika zinatakiwa kupakua mizigo na kuondoka lakini sasa hakuna nafasi, mgomo huu ukiendelea hata sisi tutashindwa kufanya kazi,” alisema.
Kutokana na mgomo huo,  meli 15 zipo nje ya bandari zinakitarajiwa kuingia, lakini zimeshindwa kuingia kwa kuwa   ipo mizigo inayotakiwa kushushwa na kupakiwa kwenye malori kwa ajili ya safari.
“Nje ya bandari zipo meli tano za makontena, meli tisa za mizigo mchanganyiko na moja ya mafuta zinazotarajiwa kuingia,” alisema Janeth.
Katika meli hizo kwa mujibu wa Janeth, tisa ni za mizigo mchanganyiko, mbili za ngano, nne za magari, moja ya mbolea na mbili za vyuma.
Mbali ya hizo, bandarini zipo meli tatu za makontena ambazo zinatakiwa kushusha mzigo na kupakiwa kwenye malori na hazijashusha kwa kuwa bandari imejaa mbolea.
Akizungumzia uwezekano wa kutokea hasara, Kaimu Meneja wa Mafuta, Kapteni Abdull Mwingamlo, alisema endapo mgomo huo utaendelea watakaoathirika zaidi ni walaji.
Alisema kuwa upo utaratibu wa wanaokodi meli kukubaliana siku za kushusha mzigo na zinapozidi, hutoza dola 20,000 hadi 30,000 kwa siku ambazo ni gharama za ucheleweshaji zitakazopelekwa moja kwa moja kwa mlaji.
“Meli zinapoingia lazima mizigo yake iingie kwenye malori ili iondoke, ile ya mbolea makontena yake tumeyapanga bandarini na kumejaa hatuna sehemu ya kuweka mizigo mingine...kwa kuwa mzigo huo haukustahili kukaa bandarini unachukua nafasi na kuzuia shughuli nyingine,” alisema.
Alisema Bandari inapata mapato kutokana na kutoza gharama za mtumiaji wa bandari, hivyo meli inapokaa muda mrefu bandarini inazuia nyingine kuingia.
Kapteni Mwingamlo alisema kwa upande wa mafuta, meli hazijaathirika kwa kuwa yanapopakuliwa, hupelekwa moja kwa moja kwenye maboya na meli za magari nazo hazijaathiriwa kwa kuwa yenyewe hayatumii sana usafiri wa malori.
Akizungumzia mradi wa boya, Ruzangi alisema kuwa tangu boya hilo lizinduliwe Novemba 2012, limehudumia mafuta safi tani 1,529,411 na tani 513,787 za mafuta ghafi, wakati mafuta yaliyohudumiwa na Kitengo cha Mafuta Kurasini(KOJ) kwa muda huo ni tani 1,503,298.
“Kukamilika kwa mradi huu kunaiwezesha bandari kuhudumia meli kubwa zenye uwezo wa kubeba mzigo tani 150,000 hivyo kuongeza tija katika kuhudumia meli za mafuta. Tofauti na boya la awali, SPM inapokea na kusukuma mafuta safi na ghafi kwa wakati mmoja,” alisema.
Pia alisema TPA inatarajia kutekeleza mradi wa SPM awamu ya pili kati ya 2014 na 2016 na itahusisha ujenzi wa matangi ya kupokea mafuta kwa muda na kugharimu dola za Marekani milioni 60 sawa na Sh bilioni 96 za Tanzania.

No comments: