![]() |
| Moshi Chang'a. |
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Moshi Chang’a, ameng’aka na kudai kuwa halmashauri mpya ya wilaya ya Kalambo imehujumiwa katika ugawaji wa mali, madeni na rasilimali watu na kuelezea msimamo kuwa ni kutaka mgawo huo ufanyike upya.
Chang’a alitoa lawama hizo wakati akifungua kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, kilichofanyika juzi mjini Matai, yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.
“Wala sitaona aibu kusema haya ukweli ni kwamba halmashauri hii mpya ya wilaya ya Kalambo tumepigwa bao…hatukupewa chochote katika mgawo wa rasilimali baada ya halmashauri mama ya wilaya ya Sumbawanga kugawanywa na kuzaliwa hii yetu.
“Sasa badala ya ujio wa halmashauri hii mpya kuwa baraka, umegeuka kuwa adhabu tena ni sawa sasa na jehenamu kwani fedha zote za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya halmashauri hii zimebakia katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga,“ alisisitiza Chang’a.
Changamoto nyingine aliyosema Chang’a ni miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo mpya ya Kalambo ambayo imebainika kutekelezwa chini ya kiwango, ambayo alidai kuwa mikataba yake ilisainiwa kabla ya kugawanywa kwa halmashauri mama na kuzaliwa kwa halmashauri hiyo mpya ya Kalambo.
“Hata mamilioni ya fedha za usimamizi wa miradi ya maendeleo ya halmashauri hii mpya ya wilaya ya Kalambo, yapo katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga.
“Tunaomba yasiendelee kutunzwa huko kwani kuna taarifa zimeanza kuliwa na wajanja kwa kuhonga wanawake mjini Sumbawanga,“ alidai Chang’a.
Alisema hata waraka unaoonesha mgawo wa rasilimali hizo halmashauri ya Kalambo haijapatiwa kwa maelekezo kuwa haupo.
Aliwaeleza madiwani hao kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa umeshataarifiwa juu ya kadhia hiyo, sasa kinachofuata ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutaarifiwa juu ya kero hiyo ili ipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Wakati huo huo, madiwani wa halmashauri hiyo ya Kalambo walimchagua diwani wa kata ya Msanzi, Faustine Mwanisenga (CCM) kuwa Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo akiwa mgombea pekee baada ya Chadema kuamua kukwepa kuweka mgombea.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na kufariki dunia kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Henry Kacheche, Septemba 13, mwaka huu.

No comments:
Post a Comment