Wednesday, October 23, 2013

KAMANDA JAMES KOMBE AFARIKI DUNIA, MWILI WA UNCLE J WAAGWA...

Kamanda James Kombe enzi za uhai wake.
Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) mstaafu, James Kombe, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Advera Senso, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa utaratibu wa maziko unaandaliwa na Jeshi hilo kwa kushirikiana na familia.
Kombe alizaliwa mwaka 1950 huko Mwika mkoani Kilimanjaro na alijiunga na Polisi Machi 15, mwaka 1970 baada ya kuhitimu elimu ya sekondari 1969 nchini Uganda.  Alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.
Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya kupata vyeo hivyo katika mabano ni pamoja na Sajini wa Polisi (1973) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1977), Mkaguzi wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa Polisi (1991), Mrakibu Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi (1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu mwaka 2010.
Nafasi alizowahi kuzitumikia Polisi ni pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika wilaya za Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa (RPC) katika mikoa ya Lindi, Arusha na Kigoma.
Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Tanzania na hadi anastaafu alikuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania.
Wakati huo huo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, jana aliungana na waombolezaji mbalimbali kuaga mwili wa mwandishi na mtangazaji mkongwe nchini, Julius Nyaisanga, maarufu Uncle J, katika Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika viwanja hivyo, Dk Bilal alisema Nyaisanga  atakumbukwa si tu na waandishi wenzake, bali na Tanzania nzima kutokana na kazi yake na kutaka waandishi kuiga mfano wake.
Mbali na Dk Bilal, wengine waliojiunga na mamia ya wakazi wa Dar es Salaam kumuaga Nyaisanga ni pamoja na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, wanasiasa na viongozi wa dini.
Viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Reginald Mengi.
Nyaisanga alizaliwa Januari mosi 1960 katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara. Alipata elimu yake ya msingi nchini Kenya kuanzia  1970 na baadaye alimaliza elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Buhemba kabla ya kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Nyegezi mwaka 1989.
Alifanya kazi katika vituo mbali mbali vya redio na televisheni ikiwemo kituo cha  Voice of Kenya Radio, Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Radio One, Shirika la Habari la  Ujerumani na Abood Media alipokuwepo mpaka kifo kilipomkuta.
Alifariki Jumapili iliyopita asubuhi saa moja katika Hospitali ya  Mazimbu mkoani Morogoro, ambako alipelekwa kwa matibabu ya sukari na shinikizo la damu.

No comments: