Monday, October 21, 2013

MENEJA WA SHIRIKA LA TAIFA LA USAGAJI AIBUKA NA KUDAI HAJAKABIDHI MALI...

Dk James Wanyancha.
Aliyekuwa Meneja wa Shirika la Taifa la Usagishaji (NMC) mkoani Arusha, ameibuka na kuomba asihusishwe na upungufu wowote utakaoibuka ndani ya shirika hilo kwa kuwa hajakabidhi rasmi mali.
Meneja huyo, Joshua Mtinangi akizungumza kwa simu hivi karibuni akiwa njiani kwenda mkoani Singida, alidai hakukabidhi mali kwa kuwa hakuridhishwa na baadhi ya mambo, hivyo kutaka taratibu zifuatwe.
Alidai hayo ikiwa ni siku chache baada ya kampuni ya kununua, kuuza na kusaga mazao ya Monaban ya jijini hapa iliyokuwa ikikiendesha kinu cha NMC, kuanza kujisimamia wakati ukisubiriwa uamuzi wa Serikali wa ama kukiuza au kukikodisha kiwanda hicho.
Ingawa hakutaka kuelezea undani wa utata aliouona na hata kushindwa kukabidhi mali za shirika hilo, alidai; “Nashukuru nimestaafishwa na kulipwa kila kilicho changu, ila nasikitika sijakabidhi mali za shirika.
“Cha ajabu hata kabla sijakabidhi, yamebandikwa matangazo kwamba sitakiwi kuonekana tena eneo la ofisi. Hili linanishangaza sana kwa sababu wakati wa uongozi wangu kulikuwa na mali nyingi za shirika na zile za kampuni za bia kama TBL na Serengeti. Lakini pia kuna upungufu nilikuwa nashughulikia kuanzia madeni ya shirika kutoka kwa mwekezaji wa sasa na mambo mengine, sijui haya yataishiaje,” alidai.
Mkurugenzi Mkuu wa Monaban, Philemon Mollel akizungumzia kupigwa marufuku kwa Mtinangi kukanyaga ofisi za NMC, alidai hana taarifa za aliyemzuia na kuongeza kuwa, yeye anaendelea na majukumu yake.
“Mtinangi hakuwa mwajiri wangu, siwezi kumzungumzia. Labda mwajiri wake ndiye anayeweza kujua kwa nini amemuondoa, mimi nahangaika na majukumu yangu kuhakikisha nazalisha chakula kwa wingi na kuwa mfano kwa wafanyabiashara wa Kitanzania. Sidaiwi na sina tatizo lolote na mmiliki wa mali ndiyo maana bado nipo hapa,” alidai.
Sakata la NMC Arusha linatajwa kuwa na`vitimbi vingi licha kuelezwa kuwa mwaka 2008 Baraza la Mawaziri liliamuru mali zote za NMC ikiwa ni pamoja na vinu vya kusagisha unga wa mahindi na ngano, maghala na vihenge vikabidhiwe kwa Bodi ya Nafaka iliyoundwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge.
Hata hivyo, kufikia sasa Bodi hiyo kwa mujibu wa Mwenyekiti wake, Dk James Wanyancha haijakabidhiwa mali za NMC Arusha, hivyo kufanya tawi pekee ambalo mali zake hazijauzwa.

No comments: