Monday, October 21, 2013

FASTJET YAZINDUA SAFARI KWENDA AFRIKA KUSINI...

Moja ya ndege za FastJet.
Shirika la Ndege la FastJet limezindua safari ya kwanza ya Kimataifa kutoka Dar es Salaam kwenda Johannesburg, Afrika Kusini.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Ed Winter akiahidi shirika hilo kuzindua safari zaidi.
Ndege ya kwanza ya FastJet ilifanya safari yake kwenda kutoka Uwanja wa Ndege ya Kimataifa wa Julius Nyerere kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa O.R. Tambo mwishoni mwa wiki, huku safari hizo zikitarajiwa kufanyika mara tatu kwa wiki, Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kabla ya kuwa kila siku karibuni.
Winter alisema; “Kwa miaka mingi usafiri wa anga baina ya Dar es Salaam na Johannesburg umekuwa ukiendeshwa na shirika moja tu la ndege na hivyo hatua hiyo kusababisha kukosekana kwa ushindani na kuwaathiri abiria.
“Ni  kutokana na ukosefu huo wa ushindani safari ya saa 14 angani kutoka Dar es Salaam kwenda Ulaya imekuwa ikitozwa bei sawa na ile ya kwenda Afrika Kusini umbali wa saa tatu na nusu tu angani, jambo ambalo haliingii akilini,” alisema Winter.
Alisema Shirika la FastJet litahakikisha kuwa linarekebisha kasoro hiyo ili kuwawezesha abiria kulipa bei ya chini hatua itakayowavuatia watu wengi kusafiri kati ya miji hiyo miwili inayokuwa kwa kasi kibiashara kwa shughuli mbalimbali kama matembezi au biashara.
Alisema Watanzania wanaweza kutumia fursa ya kusafiri baina ya miji hiyo mikubwa kutokana na unafuu wa gharama za usafiri lakini pia kutokana na raia wa nchi hizo kutohitaji viza za kuishi katika nchi hizo endapo watakaa kwa muda usiozidi siku 90.
“FastJet inaahidi kutoa huduma hii ya usafiri katika uwazi lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa abiria wanalipa sawa na huduma wanayopatiwa na si kunyonywa kama inavyofanywa na mashirika mengine yanayotoa huduma kati ya miji hiyo miwili,” alisema Winter.
Ofisa Mtendaji Mkuu huyo wa Fastjet alisema kutokana na Shirika moja kushikilia njia hiyo kwa muda mrefu bila kuwa na kampuni pinzani, ni wakati muafaka kwao hivi sasa kukubali kukabiliana na changamoto zitakazotokana na FastJet kuingia katika safari hiyo na kutoza gharama nafuu.

No comments: