![]() |
| Godbless Lema. |
Mbunge wa Arusha, Godbless Lema imefutiwa kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili baada ya upande wa mashtaka kusema hauna nia ya kuendelea na kesi mahakamani hapo.
Lema alikuwa akidaiwa kufanya uchochezi kwa wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha, kiasi cha kuwafanya wamzomee Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na hivyo kuzuka vurugu.
Kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Devotha Msofe wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, lakini baada ya kuingia mahakamani, Wakili wa Serikali Elianenyi Njiro, aliomba ifutwe.
Alisema upande wa mashitaka umeona kuwa hauna nia ya kuendelea na shauri hilo.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, hakimu alikubaliana nalo; akamweleza mshitakiwa kuwa yupo huru kuanzia muda huo.
"Mshtakiwa upo huru kuanzia sasa, lakini kama upande wa mashitaka utaona kuna haja ya kuendelea na shauri hili unaweza kukamatwa, lakini kwa sasa mahakama inakuachia huru," alisema.
Awali, Wakili Method Kimomogoro, anayemtetea Lema aliwakilishwa mahakamani hapo na Wakili John Lundo.
Akisomewa maelezo ya awali, Julai 10 mwaka huu mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Elianenyi alidai Aprili 24 mwaka huu, Lema akiwa eneo la Freedom Square la IAA alifanya kosa la uchochezi wa kutenda kosa kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Elianenyi, alidai Lema aliwaeleza wanafunzi wa chuo hicho kwamba 'Mkuu wa Mkoa amekuja kama anakwenda kwenye send-off, hajui Chuo cha Uhasibu mahali kilipo wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hiki'.
Akizungumza nje ya mahakama baada ya kesi yake kufutwa, Lema alisema, kesi hiyo ilikuwa ya kutengenezwa na ndio maana mashahidi wengi walikuwa polisi.

No comments:
Post a Comment