Thursday, October 3, 2013

CHAMA CHA WALIMU TANZANIA CHAGAWANYIKA MAKUNDI MANNE...

Ezekiah Oluoch.
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kinakabiliwa na mgogoro wa ndani kwa ndani, ambapo sasa kuna makundi manne ya walimu, yaliyojitambulisha kutaka kujitoa ndani ya chama hicho na kuunda chama kingine.

Ndani ya chama hicho kuna wanachama ambao ni wafuasi wa   Mtandao wa Walimu Tanzania (TTN), Kamati ya Taifa ya Wanachama wa CWT, Umoja wa Maofisa Elimu Tanzania (UMET) na kundi la walimu wa shule za msingi Ukerewe wanaoandaa chama chao na wote wanapanga kujitoa CWT.
Juzi akiwa Iringa, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema Umoja wa Maofisa Elimu Tanzania (UMET), ni kundi mojawapo linalotaka kujitoa katika chama hicho, lakini hawana usajili.
Alitamba kuwa CWT haina hofu na tishio la baadhi ya walimu nchini kutaka kuanzisha chama mbadala cha walimu, huku akijibu hoja mbalimbali za makundi mengine yanayotaka kujitoa.
Kundi la pili ni Kamati ya Taifa ya Wanachama wa CWT, iliyopo Dar es Salaam, inayoungwa mkono na walimu wa shule za msingi na katika hoja zake za kujitoa CWT, wanasema wanataka usawa kwa kuwa wao ni wengi.
Katibu wa Kamati hiyo, Joseph Beda akizungumza na mwandishi hivi karibuni alisema; "Tunachotaka ni sisi walimu wa shule za msingi, tuwe na nafasi kwenye chama hiki. Kwanza sisi ndio wengi na michango asilimia 75 na zaidi, ni ya walimu wa shule za msingi.
"Kama hatusikilizwi tunajitoa CWT na kuunda chama chetu, lakini hata tukijitoa, lazima tutadai haki zetu za michango tuliyokatwa huko nyuma," alisisitiza.
Alisema kwa sasa ndani ya chama hicho, hakuna usawa, nafasi nyingi kuanzia makao makuu ya chama hicho hadi wilayani, zinatolewa kwa wengine huku walimu wa shule za msingi wakiachwa jambo ambalo si haki, kwa kuwa wapo walimu wengi wenye uwezo, sifa na elimu.
Kundi la tatu la walimu wanaotaka kujitoa ni TTN, ambao kwa mujibu wa  Beda, kundi hilo ni chama halali chenye usajili, na malengo yake ni sawa na Kamati hiyo na Mwanza kundi hilo lina takribani walimu 800 wa shule za msingi wanaotaka kujitoa.
Kutokana na urasmi wa kundi hilo la TTN, Beda alisema waliona bora waunganishe Kamati hiyo yenye wanachama Dar es Salaam na kundi hilo la Mwanza kwa kuwa malengo yao ni sawa.
Tayari kamati hiyo na TTN wamekutana katika mkutano wao wa kwanza uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, na kupitisha maazimio.
Azimio la kwanza ni kuanza kampeni ya kuhamasisha walimu wa shule za msingi, kujitoa CWT na kusimamisha makato ya michango yao kwa chama hicho, ambayo ni asilimia mbili ya mishahara yao kila mwezi.
Azimio lingine ni kukataa kwa nguvu mgomo uliopangwa na viongozi wa CWT, unaotarajiwa kufanyika mwezi huu, kwa kuwa wameona hauna tija na wala haulengi matatizo halisi ya walimu likiwamo la mishahara midogo.
Kundi la nne ni la walimu wa shule za msingi Ukerewe, ambao mwezi uliopita walitaka kuandamana kupeleka ujumbe wao kwa Serikali kwamba wanataka kujitoa CWT.
Kiongozi wa walimu hao, Mwalimu Michael Muhabi, alisema wako katika hatua za mwisho za kuanzisha chama kipya cha walimu, na waliandika barua Polisi kuomba kibali cha kuitisha maandamano, ili kufikisha kilio chao kwa Serikali.
Barua hiyo  iliyosainiwa na  Mwalimu Muhabi, ilitaja sababu za  kuitisha  maandamano hayo, ikiwemo kupinga walimu wasio wanachama   wa CWT kukatwa asilimia mbili ya  mshahara  wao kila mwezi kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa CWT.
Pamoja na kutaka fedha hizo zirejeshwe kwa walimu  husika, walimu hao pia walielezea kupinga migomo ya walimu  waliyosema haina tija na imeonekana kuwanufaisha viongozi  wa juu wa chama hicho. 
Walimu hao  walilenga  pia kushinikiza Serikali  itoe tamko juu ya ukusanyaji wa fedha  za hisa  za Benki  ya Walimu,  ambazo wanadai   hadi sasa  hatma ya kuanzishwa kwake haijulikani  hali inayowatia hofu.
Hata hivyo,  Mkuu wa  Polisi  wa Wilaya hiyo (OCD), Shitambi  Shilogile   alizuia maandamano hayo na kuwataka walimu hao    kutumia njia nyingine kupata haki zao ikiwemo kukutana katika meza  ya mazungumzo na ikishindikana, waende Mahakama ya Kazi  kwa utatuzi wa kisheria.
Mwenyekiti wa CWT wa  Wilaya ya Ukerewe,  Pastory Kabalinde  alisema  sheria za nchi zipo wazi  kwa  wafanyakazi wanaotaka  kuanzisha  chama  chao, na kama  wapo walimu  wenye nia hiyo hawazuiwi.
Katika kile kilichoonekana ni kujibu hoja hizo, Oluoch akiwa Iringa juzi alisema: "Siogopi kikundi chochote kikisajiliwa kuwa chama cha walimu; kitakachoangaliwa mwisho wa siku ni kipi kina wanachama wengi ili kiingie mikataba na waajiri."
Mbali na kauli hiyo, kiongozi huyo wa juu wa CWT alisema ni ndoto kwa wanachama wa CWT kufikiri kwamba fedha wanazochangia chama hicho, zitarudi kama gawio kwao kwani kazi yake ni kushughulikia matatizo ya walimu.
Alisema CWT ni sauti ya walimu hata kama Serikali itakataa kukaa nayo meza moja ya majadiliano, ili kupatia ufumbuzi changamoto za walimu na  kutoa mwito kwa walimu,  wasivuruge utumishi wao kwa kukubali kutumiwa kisiasa.
Akikanusha taarifa zinazohusu baadhi ya viongozi wa CWT kuchukua fedha za chama hicho bila kufuata taratibu, akidai hazina ukweli na kwamba zinakinzana na maendeleo makubwa yanayoendelea kuonekana CWT.
"Ni kawaida popote kwenye mafanikio, lazima pawepo na watu watakaoingiza majungu, lakini nataka niwaambie fedha wanazosema zinaliwa ndio zimejenga mejengo ya CWT katika mikoa 20 nchini, huku tukiwa katika hatua za mwisho za kufungua benki yetu," alisema.
Alisema hayo ni mafanikio makubwa ya uwekezaji ambayo hayawezi kufafanishwa na chama chochote cha wafanyakazi kama chao.
Oluoch alisema benki yao inayotarajiwa kuwa mkombozi mkubwa wa walimu nchini, itaitwa Mwalimu Commercial Bank na tayari imesajiliwa.
"Hadi leo (juzi) navyoongea na ninyi tuna mtaji wa Sh bilioni 11, na ifikapo mwishoni mwa Novemba, tutakuwa na mtaji wa Sh bilioni 15; kwa hiyo katika  miezi mitatu kutoka sasa, tuna uhakika wa kupata leseni na kuanza biashara," alisema.
Alionya kuwa walimu watakaonufaika na mikopo ya benki hiyo, watalazimika kuwa wanachama wa CWT.
Wakati huo huo, kiongozi huyo ameahidi kuzifanyia kazi tuhuma za matumizi mabaya ya zaidi ya Sh milioni tisa zinazoukabili uongozi wa CWT Iringa Mjini.
Katika kikao alichofanya mapema na baadhi ya wanachama wa CWT wa mjini Iringa katika ukumbi wa shule ya sekondari Mwembetogwa mjini hapa, viongozi hao walituhumiwa kutumia kiasi hicho cha fedha kwa matengenezo ya gari.

No comments: