WAZIRI NYALANDU KUPOKEA MAANDAMANO YA KUPINGA UJANGILI LEO...

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (kushoto).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, anatarajiwa kupokea Maandamano ya Kupinga Ujangili wa Tembo yaliyopewa jina la ‘Tembea kwa ajili ya Tembo’.

Maandamano hayo yaliyochukua siku 19, ambayo waandamanaji watakuwa wametembea kilometa 650 kutoka jijini Arusha  yanatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam leo asubuhi. 
Matembezi hayo ya kupinga ujangili yameandaliwa na Taasisi ya African Wildlife Trust (AWT), na lengo ni kuelimisha wananchi na ulimwengu mzima kuhusu madhara ya ujangili. Matembezi yamehusisha raia wa nchi mbalimbali duniani.
Nyalandu ambaye ndiye mgeni rasmi katika kilele cha matembezi hayo, anatarajiwa kuungana na msafara wa waandamanaji eneo la Ubungo jijini saa tatu asubuhi, na kutembea nao hadi viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo atapokea risala kutoka kwa waandamanaji.
Akizindua maandamano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki vita dhidi ya ujangili kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwatia mbaroni wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Doroth Masawe aliyehudhuria uzinduzi wa maandamano hayo alisema wizara inaunga mkono harakati zote za kupambana na ujangili kwani bila hatua madhubuti kuchukuliwa iko hatari ya wanyama kama tembo kutoweka na huo utakuwa mwisho wa utalii.

No comments: