Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako kesi hiyo inasikilizwa. |
Vigogo watatu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wanaokabiliwa na mashitaka ya ubadhirifu na wizi wa Sh milioni 100 wamepatikana na kesi ya kujibu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hakimu Mkazi Aloyce Katemana alisema hayo jana, baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi tisa pamoja na vielelezo vilivyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Washitakiwa hao ni Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo, Simon Lazaro, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi, Gerald Mango na Kaimu Mhasibu Mkuu wa Tume hiyo, Charles Kijumbe.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Katemana alisema Takukuru wamejenga kesi, hivyo washitakiwa watatakiwa kupanda kizimbani kujitetea dhidi ya tuhuma hizo.
Washitakiwa walidai kuwa watatoa utetezi wao kwa njia ya kiapo na watakuwa na mashahidi 13, ambapo wataanza kujitetea Septemba 16 hadi 18 na Septemba 24 na 25.
Ilidaiwa kuwa Lazaro akiwa mwajiriwa wa Wizara hiyo, aliwasilisha nyaraka za marejesho kwa mwajiri wake, zikionesha amepokea Sh milioni 100 kutoka Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi na kuzitumia kupima ardhi katika wilaya za Babati, Kilolo na Bariadi, pia anadaiwa kuzitumia kwa maslahi binafsi.
Katika mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka, ilidaiwa kuwa kati ya Julai 4 na Agosti 5 mwaka juzi, washitakiwa wote wakiwa waajiriwa wa Wizara hiyo, walitumia madaraka yao vibaya kinyume na Kanuni ya Fedha za Umma ya Mwaka 2004.
Kwa mujibu wa Wakili wa Takukuru, fedha hizo zilipaswa kutumika kupima ardhi katika maeneo ya Muleba mkoani Kagera, Ngorongoro, mkoani Arusha; Songea mkoani Ruvuma, Kilosa mkoani Morogoro na Mpanda mkoani Katavi.
No comments:
Post a Comment