Makao Makuu ya Chama cha Walimu Tanzania. |
Walimu wa shule za msingi wilayani Ukerewe, wanajiandaa kuanzisha chama kingine, ili wajitoe uanachama wao katika Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Kiongozi wa walimu hao, Mwalimu Michael Muhabi, alisema hayo jana alipokuwa akilalamikia hatua ya Polisi kuzuia mandamano yao yaliyotarajiwa kufanyika leo.
Kabla ya hapo, walimu hao ambao wako katika hatua za mwisho za kuanzisha chama kipya, waliandika barua Polisi kuomba kibali cha kuitisha maandamano, ili kufikisha kilio chao serikalini.
Barua hiyo iliyosainiwa na Muhabi, ilitaja sababu saba za kuitisha maandamano hayo, ikiwamo ya kupinga walimu wasio wanachama wa CWT kukatwa asilimia mbili ya mshahara kila mwezi kwa ajili ya kugharimia uendeshaji wa CWT.
Pamoja na kutaka fedha hizo zirejeshwe kwa walimu husika, pia wanapinga migomo ya walimu waliyosema haina tija na imeonekana kunufaisha viongozi wa juu wa chama hicho.
Walimu hao walilenga pia kushikiza Serikali itoe tamko juu ya ukusanyaji fedha za hisa za Benki ya Walimu, ambazo wanadai hadi sasa hatma ya kuanzishwa kwake haijulikani hali inayowatia hofu walimu.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Shitambi Shilogile, alisema jana wamezuia maandamano hayo kwa kuwa walimu hao wanaweza kutumia njia nyingine kupata haki zao.
Shilogile alisema madai yao yanaweza kumalizwa kwa njia nyingine ikiwamo kukutana katika meza ya mazungumzo na ikishindikana waende Mahakama ya Kazi kwa utatuzi wa kisheria.
Katika taarifa ya Jeshi hilo ambayo nakala yake alipewa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya na OCD, Kamanda Shilogile alionya yeyote atakayekaidi amri ya Polisi, atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumzia amri hiyo, Muhabi ambaye ni Mratibu wa maandamano hayo, alitaka Polisi ifanye kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria.
Alisema zuio la Polisi ni kinyume cha Katiba inayotoa haki ya kuandamana. Alisema hatua hiyo ni sawa na kuahirisha tatizo.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Mery Tesha aliyetakiwa kupokea maandamano hayo, alitaka walimu kuepuka vurugu hasa maandamano, kwa kuwa zipo njia nyingine za kudai haki zao ikiwamo kufanya mazungumzo.
Rais wa CWT, Gratian Mkoba, akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa simu, alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo hadi atakapopata madai ya walimu hao.
Mwenyekiti wa CWT wa Wilaya ya Ukerewe, Pastory Kabalinde alisema sheria za nchi ziko wazi kwa wafanyakazi wanaotaka kuanzisha chama na kama wapo walimu wenye nia hiyo hawazuiwi.
No comments:
Post a Comment