MCHUNGAJI APANDISHWA KIZIMBANI KWA KUHIFADHI WAHAMIAJI HARAMU...

Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam.
Mchungaji wa Kanisa la Life Change Chapel lililopo Sinza, Blessing Dangana (36) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kuwahifadhi Raia wa Nigeria waliokuwa wanaishi nchini bila kibali.

Mchungaji Dangana ambaye pia ni raia wa Nigeria alifikishwa mahakamani hapo pamoja na Wanigeria wenzake wanne, Offer Nduguisi (38), Steven Irueze (28) Otika Uchenna (24) na Apostel Chinembeze (33) ambao walikuwa wahudumu kanisani kwake.
Walifikisha mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo na kusomewa mashitaka na Wakili Namtelo Simba kutoka Idara ya Uhamiaji.
Wakili Simba alidai katika mashitaka yanayomkabili Mchungaji Dangana kuwa Septemba 10 mwaka huu katika kanisa hilo, alikutwa akiwa amewahifadhi raia wanne wa Nigeria walikuwa wakiishi nchini bila kuwa na kibali.
Katika mashitaka yanayowakabili washitakiwa wengine, ilidaiwa kuwa siku hiyo walikutwa wakiishi na kufanya kazi nchini bila kuwa na kibali.
Mchungaji Dangana na Chinembeze walikana mashitaka na washitakiwa wengine walikiri.  Washitakiwa wote walirudishwa rumande na kesi imeahirishwa hadi Septemba 23 mwaka huu, watakaposomewa maelezo ya kesi.

No comments: