Wabakaji hao wakitolewa mahakamani baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo, huku baadhi ya wananchi wakishangilia hukumu hiyo. |
Wanaume wanne jana wamehukumiwa kifo kwa kuhusika na shambulio la ubakaji na mauaji ya msichana kwenye basi mjini Delhi.
Akshay Singh Thakur, miaka 28, Pawan Gupta, miaka 19, Vinay Sharma, miaka 20 na Mukesh Kumar, miaka 26, walitiwa hatiani kuhusiana na shambulio hilo la kutisha Desemba ambalo lilipelekea wito kila kona kutaka wanyongwe.
Jaji Yogesh Khanna, ambaye aliwatia hatiani wanaume hao kwa shambulio la ubakaji na 'kusababisha' mauaji mapema wiki hii, alikataa ombi la mwanasheria wao la kuwapunguzia adhabu wateja wake hao.
Shangwe zililipuka kutoka kwenye umati wa watu nje ya mahakama hiyo ya Delhi pale wanasheria walipotoka nje kwa kasi na kutangaza hukumu hiyo iliyotolewa kutokana na shambulio hilo la Desemba mwaka jana, ambalo liliibua maandamano makubwa kote nchini India na midahalo kadhaa kuhusu uhalifu dhidi ya wanawake.
"Hii imeshitua jamii nzima ya wapenda amani," Jaji Yogesh Khanna alisema, akiwahukumu wanaume hao adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
"Katika nyakati hizi huku uhalifu dhidi ya wanawake ukiongezeka, mahakama haziwezi kugeuka vipofu mbele ya makosa hayo ya kutisha."
Hukumu hiyo ilikuwa moja ya vipimo vikubwa kabisa kwa miaka kadhaa ya mtazamo wa kweli kinzani ya India kuelekea hukumu ya kifo.
Majaji wa nchini humo wanatoa, kwa wastani, hukumu 130 za kifo kila mwaka lakini India imeshaua watu watatu tu katika miaka 17 iliyopita.
Licha ya kusita kwake kutekeleza hukumu hizo, mwaka jana India ilipiga kura dhidi ya upitishwaji muswada wa Umoja wa Mataifa uliotaka ruhusa ya kusitishwa kwa muda adhabu za kifo.
Wanasheria wa watuhumiwa wote wanne walisema watakata rufani, kitu kinachomaanisha utekelezwaji hukumu zao unaweza kuwa miaka kadhaa ijayo. Kesi hii itakwenda katika Mahakama za Juu na kisha Mahakama Kuu.
Endapo zitathibitisha hukumu hizo, uamuzi wa mwisho utamtegemea Rais, ambaye ana mamlaka ya kufanya huruma.
Mmoja kati ya wanne hao, mwalimu wa gym Vinay Sharma, alimwaga machozi wakati akitolewa nje ya mahakama hiyo, ambako polisi wakiwa na vifaa vya kukabiliana na ghasia walijipanga kuzuia umati mkubwa wa wananchi.
Mwathirika huyo, ambaye alibakwa kwa saa moja na kujeruhiwa kwa nondo ndani ya basi lililokuwa kwenye mwendo, amekuwa alama ya hatari wanazokabiliwa nazo wanawake katika nchi ambayo ubakaji unaripotiwa kwa wastani wa kila dakika 21 na mashambulio ya tindikali na kesi za kukera yameshika kasi.
Mwanamke huyo, ambaye ametokea katika familia ya maisha ya kati na kufanya kazi kwenye kituo cha mawasiliano wakati akiwa anaendelea na masomo, hajatajwa kutokana na sababu za kisheria, lakini vyombo vya habari vya India vimempachika jina la Nirbhaya, neno la Kihindi linalomaanisha asiye na hofu.
"Leo tunaweza kupumua kidogo kirahisi," alisema mama wa mwathirika huyo, ambaye alimkumbatia ofisa mmoja wa polisi nje ya mahakama hiyo baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo. "Natumaini hukumu hiyo itawatisha watu kufanya makosa kama haya kwa siku za usoni."
Mawakili wa utetezi wameiasa mahakama hiyo kupuuza walichosema kimezagaa na shinikizo la kisiasa kutoa adhabu hiyo kali zaidi.
"Huu sio ushindi wa ukweli. Ila ni pigo kwa haki," wakili wa utetezi A.P. Singh aling'aka kwa jaji wakati hukumu hiyo ikisomwa.
"Jaji amechukua uamuzi huo chini ya shinikizo la kisiasa bila kujali uhalisia," aliwaeleza waandishi baadaye.
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo, Sushilkumar Shinde, alikanusha kwamba kulikuwa na muingilio wa kisiasa, akisema: "Hakuna mamlaka yoyote ya sheria inayoathiriwa na serikali."
No comments:
Post a Comment