SHERIA YA KUWABANA WAFANYABIASHARA WA DAWA ZA KULEVYA YAANZA KUTUNGWA...

Sehemu ya dawa za kulevya iliyowahi kukamatwa hapa nchini.
Serikali imeanza kubana wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini kwa kutunga sheria mpya ya dawa hizo ili kukabiliana kikamilifu na kuzuia mianya inayokwamisha jitihada za udhibiti wa tatizo hilo nchini.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali kuona sheria iliyopo haikidhi kikamilifu udhibiti wa tatizo hilo, pamoja na kusababisha uamuzi katika baadhi ya kesi hizo kuacha hisia mbaya na kuleta utata kwa jamii.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi na kubainisha kuwa kuanzia jana hadi mwisho wa mwezi ujao,  Serikali imeanza kupokea maoni ya wadau.
“Serikali imeamua kushirikisha wadau wengi kwa kuwa wana uelewa wa kutosha kuhusu tatizo la dawa hizo, ili kuchambua sheria hiyo na kutoa michango, maoni na ushauri utakaowezekana kupatikana kwa sheria madhubuti itakayokidhi hali halisi ya tatizo na kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini,” alisema.
Alisema wanapokea msaada wa wananchi wote hata kama hayajawekwa kisheria, wao watayaweka ili kuhakikisha inatungwa sheria itakayodhibiti dawa.
“Maoni ya wadau tutayapokea kwa awamu mbili kuanzia leo (jana) hadi Oktoba ambapo tutatoa Muswada na kabla haujaenda bungeni wadau watatoa mapendekezo tena ndipo upelekwe bungeni,” alisema Lukuvi.
Alisema kuna vifungu vingi katika sheria ya mwaka 1995 vinaguswa na kuhitaji marekebisho kama kuondoa thamani za dawa za kulevya na kutumia uzito, kuongezwa kwa adhabu katika vifungu vingi, kuwa na chombo kipya chenye mamlaka kamili ya kuchunguza, kukamata na kupeleleza.
“Serikali imeona umuhimu wa kufuta sheria ya sasa na kutunga nyingine itakayozingatia mabadiliko yanayohitajika, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kushughulikia makosa hayo ili kurahisisha usikilizwaji wa kesi,” alisema Lukuvi.
Alisema katika kuanzisha chombo mahususi cha kuzuia na kupambana na tatizo hilo, Serikali inatarajia katika sheria hiyo kukipa mamlaka ya kutosha ya kupambana na matumizi  na biashara ya mihadarati.
Alitaja upungufu uliopo katika sheria iliyopo kwa kutoa mifano ya kifungu cha 21 kinachohusu wafadhili wa biashara hiyo kutoa adhabu ndogo licha ya kuwa ndio wamiliki na wanaostahili adhabu kali.
Alisema adhabu iliyopo ni faini ya Sh milioni 10 au kifungo cha maisha jela, huku ikimpa uhuru Jaji au Hakimu kutoa uamuzi wa kifungo au kumtoza faini mtuhumiwa kadri anavyoona inafaa, jambo ambalo kutokana na kukithiri kwa biashara hiyo, ni rahisi kulipa faini.
Lukuvi alisema kifungu kingine ni cha 12 kinachohusu uzalishaji na biashara haramu ya dawa hizo mashambani kama bangi na mirungi, kinatoa adhabu ndogo ya faini ya Sh milioni moja tatizo ambalo ni kubwa, kwani kilimo cha bangi kinakithiri.
Pia alisema sheria hiyo haibainishi wazi jinsi ya kulinda watoa taarifa za siri kuhusu biashara hiyo wala hatua za kuchukulia watendaji wanaovujisha taarifa hizo.
Lukuvi alizungumzia mafanikio ya jitihada za Serikali kukabiliana na biashara hiyo kuwa, katika kipindi cha mwaka 2009 hadi Septemba 7, walikamata watuhumiwa 318.
Alitaja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Arusha 144, Dar es Salaam 90, Tanga 37, Kilimanjaro 17, Mbeya 13, Morogoro tisa na Mara wanane.
Alisema kati yao watuhumiwa 149 walikamatwa na kufikishwa mahakamani, lakini ni kesi moja tu ndiyo iliyomalizika kwa washitakiwa watano kupatikana na hatia na kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 25 na kupigwa faini ya zaidi ya Sh bilioni 1.4 kila mmoja, ikiwa ni kesi kubwa ya washitakiwa kupewa adhabu kali.
Alisema kesi kubwa za dawa za kulevya zilizo mahakamani ambazo thamani yao ni zaidi ya Sh milioni 10 kuanzia mwaka 2010 ni Dar es Salaam 50, Kilimanjaro 11, Arusha saba, Tanga sita, Mbeya na Morogoro watatu kila mmoja na Pwani, Mwanza na Lindi kesi moja moja.
Alisema kati ya Januari na Machi kilo 12 za heroin zilikamatwa na kati ya mwaka 2008 na Septemba mwaka jana kilo 352.3 za cocaine zilikamatwa huku Januari na Machi mwaka huu kilo tatu za dawa hizo zilikamatwa.
Lukuvi alisema katika kupunguza matumizi ya mihadarati, tiba imekuwa ikitolewa na hadi mwaka 2012 watumiaji 836 walipewa matibabu huku kituo cha tiba kikijengwa   Itega, Dodoma kwa ajili ya matibabu na urekebishaji tabia kwa watumiaji wa dawa hizo.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa aliyefuatana na Lukuvi alisema watuhumiwa 261 walikamatwa kutokana na taarifa za kufanya biashara za dawa hizo, lakini hakukuwa na vielelezo.
Alisema kutokana na hali hiyo, licha ya kuwa na uhakika, waliomba Mahakama kula kiapo ambapo wamekuwa chini ya mahakama kwa muda wa miaka mitatu hadi sita ili kujirekebisha.
Akizungumzia suala la Watanzania wanaokamatwa nje ya nchi alisema kesi zinasikilizwa na hukumu kutolewa katika nchi husika na suala la kurudishwa nchini ni baada ya hukumu na ni ikiwa nchi husika ina mkataba na Tanzania wa kubadilishana wafungwa.

No comments: