Basil Mramba. |
Aliyekuwa mfanyakazi wa Benki Kuu (BoT), Kesisia Mbatia (61) ameieleza Mahakama kuwa Waziri wa zamani wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba hakuhusika katika mchakato wa kuitafuta kampuni ya kukagua migodi ya madini ya Alex Stewart.
Kesisia alidai kuwa mchakato wa kumtafuta mkandarasi huyo ulifanywa na kamati ambayo ilichaguliwa na BoT baada ya kupata maelekezo kutoka kwa aliyekuwa Gavana, Daudi Balali.
Alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.5 kutokana na kuisamehe kodi kampuni hiyo, inayomkabili Waziri Mramba na wenzake.
Kesisia ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, alidai kuwa, kamati ilikuwa na watu watano, akiwemo ofisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, maofisa wawili kutoka BoT na mshauri wa Gavana na baadaye waliongezeka wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Alidai Gavana alimpa mamlaka ya kusimamia kamati hiyo kwa ajili ya kutafuta kampuni yenye uwezo wa kukagua madini ya dhahabu, walitafuta kampuni kwa njia ya mtandao na kupata 21 baada ya kufanya upembuzi kwa kuzingatia vigezo zilibaki tano.
Aliendelea kudai kuwa waliwatumia barua, lakini walipata majibu kutoka kampuni mbili ambazo moja ilidai malipo yake yatakuwa asilimia mbili ya thamani ya dhahabu na Alex Stewart walitaka asilimia 1.9, wakaipendekeza kampuni hiyo ambayo ilitaka malipo ya asilimia ndogo zaidi.
Alidai katika mchakato wote walikuwa wakiandika ripoti na kupeleka kwa Gavana na hata baada ya kumaliza kufanya mchakato huo na kupata mzabuni huyo, walipeleka taarifa kwa Gavana.
Akihojiwa kuhusu Mramba kuhusika katika kumpata mzabuni huyo alidai “sijui na siwezi kujua kwasababu kamati yetu ndiyo ilihusika, na baada ya kumaliza mchakato tuliipendekeza kampuni hiyo na kuandika ripoti kwa gavana”.
Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, 2004, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 kwa kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza kinyume cha sheria.
No comments:
Post a Comment