Gratian Mukoba. |
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kinazidi kupata upinzani kutoka kwa wanachama wake hasa wa shule za msingi, ambapo sasa imeundwa Kamati ya Taifa ya Wanachama wa chama hicho ya kudai haki za walimu.
Kamati hiyo inakutana leo kujadili malalamiko yaliyowasilishwa kwa menejimenti ya chama hicho miaka miwili iliyopita bila kufanyiwa kazi na inatarajiwa kutoa tamko zito dhidi ya viongozi wa CWT baada ya kikao hicho.
Hata hivyo, chama hicho kimebainisha kuwa madai na malalamiko ya Kamati hiyo, hayana tija kwa kuwa baadhi ya mambo yanayodaiwa hayawezi kufanyiwa kazi, kwani yako mahakamani na mengine yanatekelezeka chini ya utaratibu wa chama hicho wa vikao.
Akizungumza na mwandishi Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Frederick Kuboja, alisema Kamati inajiandaa kufanya kampeni shule kwa shule, kuhamasisha walimu kuupinga uongozi wa CWT kwa kuwa hadi sasa haujafanikisha mahitaji yoyote ya wanachama.
"Hata hili suala la mgomo linalodaiwa kuwa utafanyika tena Oktoba, naweka wazi kuwa sisi walimu hatutashiriki, tumechoshwa na migomo isiyo na tija, tangu tuanze kugoma hakuna faida yoyote zaidi ya viongozi kutuchonganisha na waajiri," alisisitiza.
Alisema Kamati hiyo Mei ilimwandikia barua Rais wa Chama hicho, Gratian Mukoba na kumweleza masikitiko yao juu ya CWT kuanza kukosa dira na dhima ya kukomboa walimu Tanzania na badala yake kupitia Katiba mpya toleo la tano la mwaka 2009 imekuwa ikijali wanachama viongozi na watumishi walioajiriwa.
"Katiba hii tumesema tunataka ifanyiwe marekebisho, kwani uandikwaji wake haukushirikisha wanachama wa chini, ulianzia juu ya mkutano mkuu na imekuwa ikitoa nafasi kwa viongozi wa chama kujijengea himaya na matabaka ya wanachama washika chaki na viongozi wanaofaidi matunda, hii ni kuwafanya wenzao mtaji," alisisitiza.
Kuhusu Katiba hiyo, Kuboja alisema imeondoa demokrasia ya ukweli ndani ya chama hasa katika eneo la ushirikishwaji na uamuzi kutokana na Katiba kutotoa fursa kwa wanachama wa kituo cha kazi kukutana katika vikao vinavyotambuliwa na kujadili kwa uwazi masuala yanayowahusu.
Alisema Katiba hiyo inatoa utaratibu mbovu wa upatikanaji viongozi wa chama ambapo Katibu Mkuu anateuliwa badala ya kuchaguliwa na wanachama na haisemi mwanachama anapostaafu ananufaikaje na vitega uchumi vya chama ambavyo anachangia.
"Lakini pia pamoja na tatizo la Katiba, tuna wasiwasi na viongozi hawa kutokana na ukweli kuwa kuna usiri mzito wa wanachama kutopewa taarifa ya mapato na matumizi yatokanayo na ada, vitega uchumi na misaada," alisema.
Alisema pia viongozi wa chama wamekuwa wakiendelea kukata walimu ada za uanachama bila kuzingatia Waraka wa Serikali unaotoa uhuru kwa mtumishi kuchagua chama chochote cha wafanyakazi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Katibu Mwenezi wa Kamati hiyo, Evody Kanyaiyangiro, alisema chama kimekuwa na vitega uchumi vingi likiwamo jengo la Mwalimu House la Dar es Salaam na nyumba zilizo katika takribani mikoa 20 nchini, lakini hakuna taarifa za namna wanachama hai na wanaostaafu wanavyonufaika na vitega uchumi hivyo.
"Sasa hivi wanaanzisha benki ya walimu, tunataka wasitishe mchakato huo mara moja, vinginevyo tunakwenda mahakamani, huu ni wizi mtupu wa kuwaongeza viongozi hawa ulaji, sasa hivi wana kampuni ya walimu ya TDCL, hatujui inajishughulisha na nini na wenye hisa ni akina nani?," alihoji.
Alisema kwa sasa chama kimejikita zaidi kwenye biashara kuliko dhima ya uanzishwaji wake ambayo ni kusimamia maslahi ya wanachama, jambo ambalo ni kinyume cha sheria namba sita ya ajira na uhusiano ya mwaka 2004.
"Haya ndiyo yanasababisha walimu kuanzisha vyama vyao na kujitoa CWT, sisi tunataka uongozi wa chama hiki ushughulikie haya, ukishindwa tutapiga kampeni utolewe madarakani, na huko ikishindikana tutaanzisha chama chetu kingine, lakini tutakwenda mahakamani kudai haki zetu kupitia michango tunayokatwa," alisema.
Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alikiri uongozi wa CWT kukutana na Kamati hiyo wakati ikijiita Wanaharakati Walimu na kujadiliana mambo mengi yakiwamo mapendekezo ya kutaka Katiba ifanyiwe marekebisho.
"Sasa wakati nasi tukijadili hili la Katiba, suala hilo likapelekwa mahakamani na walimu wengine wakipinga Katiba hii kufanyiwa marekebisho, sasa sisi tungefanyaje, hatuwezi kufanya lolote kwa kuwa suala liko kwenye mikono ya sheria," alisema Oluoch.
Kuhusu madai ya mgomo, maslahi ya walimu na mapato na matumizi ya chama, alisema ni vitu vilivyo wazi na ambavyo kama kuna tatizo vinaweza kujadiliwa na kupangiwa utekelezaji ndani ya vikao vya chama.
"Lakini hili la madai kuwa eti chama kimegeuka cha biashara halina mantiki kwa kuwa sisi si chama pekee cha wafanyakazi chenye vitega uchumi, hata Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) lina nyumba takribani 20 Dodoma peke yake na sheria iko wazi kuwa fedha za wanachama zinaweza kuwekezwa kwa manufaa yao," alisema.
Alisisitiza, kuwa "Mchakato wa kuanzisha benki hautasitishwa, kwa kuwa azimio la kuanzisha benki hiyo ni la mkutano mkuu wa chama na hakuna mtu anayeweza kulipinga".
Hata hivyo, alibainisha kuwa madai yote hayo chanzo chake ni mtumishi aliye Ukerewe mkoani Mwanza ambaye chama hicho kimemsimamisha kutokana na utovu wa nidhamu, hivyo amekuwa akihamasisha na kufanya kampeni chafu dhidi ya uongozi wa CWT ili asichukuliwe hatua zaidi.
Wakati hayo yakiendelea Dar es Salaam, tayari walimu wa shule za msingi Ukerewe, wanajiandaa kuanzisha chama kingine, ili wajitoe CWT.
Kwa mujibu wa mmoja wa wanachama wa CWT Mwalimu Michael Muhabi, walimu hao wako katika hatua za mwisho za kuanzisha chama kipya, na tayari wameandika barua Polisi kuomba kibali cha kuitisha maandamano, ili kufikisha kilio chao serikalini.
Barua hiyo iliyosainiwa na Muhabi, ilitaja sababu saba za kuitisha maandamano hayo, ikiwamo ya kupinga walimu wasio wanachama wa CWT kukatwa asilimia mbili ya mshahara kila mwezi kwa ajili ya kugharimia uendeshaji wa CWT.
Pamoja na kutaka fedha hizo zirejeshwe kwa walimu husika, pia wanapinga migomo ya walimu waliyosema haina tija na imeonekana kunufaisha viongozi wa juu wa chama hicho.
Walimu hao walilenga pia kushinikiza Serikali itoe tamko juu ya ukusanyaji fedha za hisa za Benki ya Walimu, ambazo wanadai hadi sasa hatma ya kuanzishwa kwake haijulikani hali inayowatia hofu walimu.
No comments:
Post a Comment