SERIKALI KUENDELEA KUTUMIA SILAHA ZA MOTO KWA WAKAIDI...

Pereira Silima.
Serikali imesisitiza, kwamba  Jeshi la Polisi limekuwa likilazimika kutumia silaha za moto, kukabiliana na vurugu za maandamano na mikutano ya kisiasa, kutokana na wanaofanya vurugu hizo kukaidi amri halali itolewayo na Jeshi hilo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima, alisema hayo bungeni jana na kufafanua, kwamba  si nia ya Jeshi hilo kutumia silaha sehemu ambazo maandamano hayana vurugu kubwa.
Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), Silima  alisema bila utii wa sheria, Polisi hulazimika kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha, ili kutuliza ghasia hizo ambazo zinaweza kuleta uvunjifu wa amani.
Mbowe katika swali lake,  alitaka Serikali ieleze kwa nini Polisi inatumia silaha za moto kwa raia wasio na hatia akisema hivi sasa kuna matukio mengi ambayo Jeshi la Polisi tofauti na ilivyokuwa huko nyuma linatumia silaha za moto badala ya    mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.
Alisema Polisi imekuwa ikitumia silaha za moto hasa katika maandamano au mikutano inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini.
Akijibu swali hilo, Silima alisema askari Polisi anaruhusiwa kubeba silaha na kuzitumia kwa mujibu wa mahitaji,  anapolazimika kutumia silaha za moto, ni pale inapobidi kufanya hivyo.
“Kuwepo kwa polisi peke yake, inatosha kuwafanya wanaoleta vurugu kuacha kufanya hivyo kwa utii wa sheria bila shuruti, lakini wanaolea vurugu wanapokaidi kwa vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani, ndipo Jeshi la Polisi hutumia silaha kulingana na mahitaji,” alisema.
Naibu Waziri alisema kwa sasa hivi hakuna haja ya kuwa na Tume kufuatilia matukio ya Polisi kutumia silaha za moto, kwa kuwa kuna vyombo vinavyofanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio hayo, hadi hapo itakapolazimika kufanya hivyo.
Waziri alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jang’ombe, Hussein Mussa Mzee (CCM), aliyetaka kujua kama mabomu ya kutoa machozi yanayotumiwa katika matukio mengi ya vurugu yana madhara ambapo Waziri alimjibu kuwa hayana.
Pia Naibu Waziri alilazimika kufafanua tofauti ya mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha, kutokana na swali la nyongeza kutoka kwa Mzee, ambaye alisema vyote hivyo ni silaha baridi ila tofauti yake ni jinsi zilivyotengenezwa.
Alisema mabomu ya kutoa machozi yanatengenezwa kwa milipuko, wakati maji ya kuwasha ni vimiminika. Pia Waziri alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi juu ya utii wa
sheria bila shuruti, ili kuepusha vurugu hizo kupitia vyombo mbalimbali vikiwamo redio, televisheni na magazeti.

No comments: