![]() |
| Moja ya ndege za FastJet. |
Abiria waliokuwa wasafiri leo kwa ndege ya Kampuni ya FastJet kwenda Afrika Kusini, wamepigwa na butwaa baada ya safari hiyo kufutwa jana.
Jana kampuni hiyo ilikuwa ifanye uzinduzi wa safari ya Dar es Salaam-Johannesburg Afrika Kusini, na tayari ilishatangaza uzinduzi huo kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuchezesha bahati nasibu kupitia vyombo vya habari.
Hata hivyo, wakati abiria hao wakijiandaa kwa safari hiyo ghafla jana walitangaziwa kupitia vyombo vya habari na njia ya simu, kwamba safari hiyo haitakuwapo na kuahidi kurejeshea abiria hao gharama zao.
Akizungumzia hali hiyo jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa FastJet, Ed Winter, alisema hali hiyo ilitokana na Mamlaka ya Anga ya Afrika Kusini kuomba baadhi ya nyaraka muhimu kutoka FastJet.
Alisema awali kampuni hiyo ilikamilisha kila kitu muhimu kilichokuwa kinatakiwa kufanyika na kushangaa baadaye dakika ya mwisho kuona wanaulizwa kupeleka nyaraka zingine.
"Hii inakatisha tamaa kabisa, kwa kuwa hakuna kitu tulichokuwa hatujakamilisha É karibu kila kitu kilikuwa tayari na sisi tulishajiandaa kuzindua safari hii," alisema Winter.
Alisema kwa mujibu wa Mamlaka za Afrika Kusini itachukua siku kadhaa kufanyia kazi taarifa hizo muhimu na kutoa kibali kwa kampuni yake.
Pindi kila kitu kikikamilika, FastJet itafanya safari hizo kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na itaongeza huduma zake kadri mahitaji ya wateja wake yatakavyoongezeka.
Mmoja wa abiria ambao walikuwa wasafiri leo, ni Majaliwa Mbassa, ambaye alizungumza na mwandishi akisema, "Nilishakata tiketi yangu muda mrefu, maandalizi ya safari ikiwa ni pamoja na kubadilisha fedha nilishafanya, leo hii ghafla napigiwa simu kuambiwa safari haipo, nitafanya nini sasa?" Alihoji Mbassa.

No comments:
Post a Comment