Friday, September 27, 2013

AJALI ZIWA TANGANYIKA YAUA WATU 16, WAMO WATOTO 13...

Ziwa Tanganyika.
Watu 16, wakiwamo watoto 13 wenye umri chini  ya  miaka mitano, wamekufa maji baada ya mtumbwi  waliokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Tanganyika.

Ajali hiyo inayoelezwa kusababishwa na upepo mkali ziwani, ilitokea jana kati ya Kijiji cha Kipwa na Bandari ya  Kasanga kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika wilayani Kalambo.
Akizungumza kwa simu na mwandishi jana, Mganga Mkuu  wa Wilaya ya Kalambo, Dk Hosea Mang'ombe,  amethibitisha kutokea kwa  ajali  hiyo.
Dk Mang'ombe alifanunua kuwa watoto hao ni miongoni  mwa wakazi wa Kijiji cha Kipwa, waliopelekwa katika Kijiji cha Kapele wakiwa na mama zao kupewa chanjo, na baadhi yao walikuwa wamekwenda kliniki.
Kwa mujibu wa Dk Mang'ombe, miili ya watoto 13 na akinamama wawili iliopolewa jana huku mwili wa mjamzito ukiwa haujapatikana hadi jana.
Baadhi  ya  mashuhuda  wa  ajali hiyo kwa masharti  ya kutoandikwa majina yao,  walidai kuwapo uwezekano wa kuongezeka kwa idadi ya waliokufa.
"Idadi  ambayo haijafahamika ya wanawake  baadhi yao  wakiwa  wajawazito, walikuwa na watoto  hao  wenye umri  wa chini ya miaka  mitano kwenda  Kapele  kupata huduma  ya afya baadhi  walikuwa  wakihudhuria kliniki," alisema mtoa habari huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda,   alisema uchunguzi  wa awali  unaonesha kuwa  chanzo  cha ajali  hiyo ni  upepo  mkali  uliovuma  katika  ziwa hilo, baada ya boti  kufika kati  ya  Kijiji  cha Kipwa na Bandari ya Kasanga.
Hata  hivyo, alisema hadi jana majina  ya marehemu   hayajapatikana. "Taarifa kamili  nitawapa  kadri nitakavyokuwa  nikizipata kwa kuwa haijafahamika  idadi   kamili  ya abiria  waliokuwa  wakisafiri  katika mtumbwi huo," alisema Kamanda Mwaruanda.
Kwa mujibu  wa Kamanda  Mwaruanda, uchunguzi  wa  ajali hiyo na juhudi za kuopoa miili bado zinaendelea kwa ushirikiano wa  wananchi  na viongozi wa vijiji vya mwambao  wa Ziwa Tanganyika.

No comments: