MHARIRI NA MWANDISHI WAKE WAKANA KUCHOCHEA MGOMO WA ASKARI...

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Washitakiwa wawili katika kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi iliyokuwa ikihamasisha askari wa majeshi nchini kutotii amri ya wakuu wao, wamekana kufanya kosa katika utetezi wao.

Washitakiwa hao, mwandishi wa habari, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda, walidai jana kuwa makala inayodaiwa ilikuwa ya uchochezi, haikusababisha uchochezi.
Akijitetea katika kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mwigamba alidai  makala aliyoandika haikusababisha uchochezi, kwa kuwa hakuna askari aliyegoma au kutotii amri ya mkuu wake baada ya kuisoma.
Alidai aliandika makala hiyo kwa lengo la kutoa maoni kwa askari wasivunje haki za kikatiba, hasa haki ya kuishi na ya kufanya mikusanyiko na maandamano.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, Mwigamba aliendelea kudai kuwa aliandika makala hayo baada ya kushuhudia wanachama na viongozi wa Chadema, wakiandamana kwa amani Januari 5 mwaka juzi, na baada ya kufika eneo la Tangi Bovu, Arusha, walikuja askari mbele yao na kufyatua risasi na kusababisha vifo vya watu watatu.
Aliendelea kudai kuwa kutokana na tukio hilo, aliona umuhimu wa kukumbusha askari wanapokuwa katika maandamano, wasimamie amani na kutotii amri zisizo halali, ikiwamo ya kuua au kupiga, kwa sababu zinakiuka Katiba.
Aliongeza kuwa, anaamini makala hayo, hayakuwa ya uchochezi kwa kuwa tangu yalipochapishwa, hakuna askari aliyegoma au kulalamika, isipokuwa askari wawili ambao walifungua kesi hiyo ambao pia walikuwa mashahidi wa upande wa mashitaka.
Kwa upande wake, Kibanda alidai kuwa alipitia makala hayo kabla ya kuchapishwa na hakuona kama ni ya uchochezi na hata baada ya kuchapishwa, hakuna askari aliyegoma.
Aidha, alidai kama makala hayo yangekuwa ya uchochezi, gazeti hilo lingefungiwa au Msajili wa Magazeti angetoa onyo kwa Mhariri Mtendaji au Naibu wake, lakini hakufanya hivyo.
Kibanda na Mwigamba wanadaiwa kuchapisha makala yaliyokuwa na kichwa cha habari: ‘Waraka maalumu kwa askari wote’.
Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi, Theophil Makunga, ambaye anadaiwa kuruhusu kampuni yake kuchapisha Tanzania Daima, ikiwa na makala hayo inayodaiwa kuwa ya uchochezi.

No comments: