MAWAZIRI WAUMBUANA MPANGO WA SERIKALI 2007 KUTENGENEZA MVUA...

Ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, mjini Dodoma.
Sakata la kutengeneza mvua kwa njia ya kitaalamu kutokana na mawingu iliyokuwa kwenye mpango wa Serikali mwaka 2007, jana lilichukua sura mpya baada ya mawaziri kutofautiana ndani ya Bunge.

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mazingira), Terezia Huvisa, alisema mvua ya kutengeneza haiwezekani, lakini akapingwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.
Lukuvi alisimama na kupinga hoja ya Waziri Huvisa,   akisema mvua ya kutengeneza ni suala la kisayansi na mvua hiyo ipo.
Kutokana na kauli zinazopingana, Mwenyekiti wa Bunge aliyekuwa akiendesha mjadala wa maswali na majibu bungeni, Jenister Mhagama alitaka mawaziri hao kukaa pamoja ili kuweka msimamo wa pamoja kuhusu jambo hilo.
Pia, kwa kutumia Kanuni namba 2, Mhagama alimruhsu Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kutoa ufafanuzi kwa kuwa alipata kushughulikia suala hilo akiwa Waziri Mkuu, ambapo alisisitiza kuwapo kwa mvua hiyo akisema ukweli ni kauli aliyotoa Likuvi.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Rachel Robert (Chadema), akiuliza swali kwa niaba ya Mbunge wa Meatu, Meshack Opulukwa (Chadema), alihoji sababu ya Serikali kutorasimisha utaalamu wa kuleta mvua kutoka kwa wataalamu wa kienyeji walio katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
Lengo la hoja hiyo iliyoelekezwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, ilikuwa kusaidia maeneo yanayokabiliwa na uhaba wa mvua, yapate mvua ya kutosha.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alisema Serikali haiwezi kurasimisha suala hilo kwa wataalamu hao, kwa kuwa hakuna utafiti uliofanyika na kuthibitisha kuwapo kwa utalaamu huo.
Hata hivyo, Waziri Chiristopher Chiza, alilazimika kusimama kutoa maelezo zaidi  akidai mvua ni suala la kisayansi ambalo halina uhusiano na mambo ya wataalamu wa kienyeji.
Alisema wataalamu hao wamekuwa wakizua utata katika maeneo mengi, ukiwamo mkoa aliozaliwa wa Kigoma.
Alifafanua kuwa wataalamu hao hutumia Sayansi ndogo ya kusoma majira ya nyakati, ambapo mawingu yenye umbo la vidole ambayo huonekana saa nane kabla ya mvua kunyesha, hufanya waganga hao kutumia ujanja huo kutabiri mvua, jambo ambalo alisema huwaletea madhara na wakati mwingine kuuawa.
Alisema kukosekana kwa mvua nchini ni matokeo ya tabianchi ambayo yanaendelea kuleta madhara katika maeneo kadhaa, lakini Serikali imekuwa ikiendeleza kilimo cha umwagiliaji katika kukabiliana na hali hiyo ikiwamo mikoa ya Shinyanga na Simiyu.
Waziri Malima alisisitiza kutumika programu mbalimbali kwa teknolojia ya kuvuna maji ya mvua na kujenga mabanio ya kuchepusha maji wakati wa mvua.
Alisema ni pamoja na kuvuna maji ya mvua katika mikoa kame kupitia utekelezaji wa programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) na mradi wa DASIP.
Hata hivyo, Malima alisema kuwapo mvua katika baadhi ya mikoa kama vile Katavi na Rukwa ambapo kiasi cha mvua ni kati ya milimeta 750 hadi 1,200 kwa mwaka, kunasaidia uzalishaji wa mazao.

No comments: