MAPYA YAFICHUKA TAZARA, WAFANYAKAZI WADAI NI MRADI WA WATU WACHACHE...

Ofisi za TAZARA, Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), wameelezea namna mamlaka hiyo ilivyogeuzwa mradi wa watu wachache, mbele ya  Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Walitoa madai yao jana kwa Mwakyembe aliyefika katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Tazara, Dar es Salaam kuwaamuru wafanyakazi waliogoma kurejea kazini, waanze kazi  mara moja baada ya Serikali kuwahakikishia malipo yao ya malimbikizo ya mishahara kuingia akaunti zao leo.
Haikuwa jambo rahisi kwa Waziri Mwakyembe kuondoka katika ofisi hizo za Tazara baada ya kumaliza kuwaeleza agizo hilo la Serikali,  kwani walimzuia wakimuomba awasikilize kilio chao.
Hatua hiyo ilimfanya Waziri Mwakyembe aliyeeleza awali kuwa na kikao kingine, kukubali kuahirisha kikao hicho ili kusikiliza kero za wafanyakazi ambao walimueleza matukio mbalimbali ya ufujaji wa fedha ambao walisema kama usipodhibitiwa, mamlaka hiyo haiwezi kujiendesha kwa faida.
Msemaji wa kwanza alikuwa Amri Hussein, ambaye alidai kuna ufisadi wa mabehewa saba ya Tazara yanayofanya kazi ya kubeba mizigo kati ya Ndola nchini Zambia na Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na fedha zinazopatikana zinaliwa na uongozi wa juu ya mamlaka hiyo.
Hussein pia alidai kuna hujuma ilifanywa Julai 25 mwaka huu na Menejimenti ya mamlaka hiyo, ambapo injini ya treni namba 1022 iliyosafirisha mzigo kwenda New Kapiri Mposhi, Zambia, ilirejea Dar es Salaam kwa kufungwa kama behewa badala ya kubeba mzigo wa kurudi nao, huku injini hiyo ikiwa na mafuta ya kutosha.
“Mheshimiwa Waziri najua hiki ninachokifanya ni hatari kwa maisha yangu, nafahamu kwamba wakati wowote naweza kumwagiwa tindikali lakini nalazimika kusema maana Tazara ni mradi wa watu na hata Serikali mlete mabilioni kwa mabilioni, hakuna kitakachofanyika zaidi na fedha hizo zaidi ya kuliwa,” alidai Hussein.
Alidai mbali ya hujuma hiyo, uongozi wa Mamlaka hiyo umekuwa ukijipangia safari za mara kwa mara zisizo na manufaa kwa mamlaka hiyo, hatua ambayo imechangia kudhoofisha mapato na kuongeza gharama za matumizi.
Kwa upande wa Waziri Mwenevyali, alifichua ufisadi uliofanyika hivi karibuni ambapo msafara wa mabehewa manne ya bidhaa za Jeshi la Zambia, yalilazimika kuongezewa mabehewa mengine ya mzigo 15 na kufanya treni yenye mabehewa 19 kusafirisha mzigo kwenda New Kapiri Mposhi kwa bei ya hasara kwa Tazara.
Alisema hujuma iliyofanyika ilikuwa ni kumshawishi msafirishaji wa bidhaa hizo kutumia makontena kwa gharama ya dola za Marekani 4,000 badala ya kutumia mabehewa ambayo gharama yake ni Dola za Marekani 7,000,  huku hatua hiyo ikiwafanya viongozi wa Tazara kuiibia mamlaka hiyo fedha.
Waziri pia alifichua hatua ya kukiukwa kwa Sheria iliyounda Tazara inayotaka shughuli za  kibiashara ndani ya Tanzania kusimamiwa na Meneja wa Mkoa wa Tanzania, na shughuli hizo kufanywa na Ofisi za Makao Makuu, hatua inayofanyika kwa makusudi ili kuiiba fedha za mamlaka hiyo na kuihujumu mamlaka hiyo.
Alielezea pia kuwepo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh milioni 100 katika Kituo cha Utengenezaji wa Kokoto za Reli cha Kongolo mkoani Mbeya, ambapo alisema ubadhirifu huo ulifanywa na viongozi wa juu wa mamlaka hiyo.
Kwa upande wake, mfanyakazi Khalid Ayumbayumba  alisema anashangazwa na hatua ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Leonard Phiri kuishi katika Hoteli ya New Afrika, Dar es Salaam huku Tazara ikilipa karibu Dola 10,000 kila mwezi tangu Aprili mwaka huu huku nyumba maalumu ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo iliyoko Masaki, Dar es Salaam ikiwa imefungwa.
Mfanyakazi huyo alisema uongozi huo pia unatumia njia ya malori ili kusafirisha mafuta kwa ajili ya injini zilizoko mikoani badala ya kutumia njia ya reli, hatua ambayo pamoja na kuwatia hasara kubwa pia imewahi kusababisha hasara kubwa baada ya mafuta hayo kuchakachuliwa kwa kuwekwa maji na baadaye kuwekwa kwa injini kabla ya kugundulika huku kukiwa na madhara tayari.
“Mheshimiwa Waziri haya yote yanafanywa ili kuliibia shirika letu fedha na hawa watu watalimaliza kabisa shirika hili pamoja na jitihada hizi mnazoendelea kuzichukua za kuliongezea uwezo shirika,” alisema.
Alizungumzia pia mkataba mbovu uliokuwa unaifanya Tazara kulazimika kusafirisha mizigo kutoka Stesheni ya Chozi iliyopo Zambia kilometa zaidi ya 800 kutoka New Kapiri Mposhi ndani ya reli ya Tazara huku, Shirika la Reli la Zambia likisafirisha mizigo hiyo kutoka New Kapiri-Mposhi hadi Chozi, hatua ambayo inaitia hasara Tazara.
Wafanyakazi hao walitumia nafasi hiyo kuwashutumu mameneja saba wa mamlaka hiyo ambao walisema awali waliwahi kusimamishwa kazi lakini wakarejeshwa baadaye, kwamba ndio kiini cha matatizo yanayoikabili Tazara hivi sasa na kumuomba Waziri Mwakyembe kuwaondoa.
Kutokana na maelezo hayo,  Mwakyembe aliwataka wafanyakazi hao kumpa muda ili kuyachunguza kwa kina kabla ya kuchukua uamuzi huku akiwahakikishia kuwa atafanya kila awezalo ili kuliwezesha shirika hilo kurejea katika umaarufu wake.

No comments: