Baadhi ya wahamiaji haramu kutoka nchini Ethiopia wakiwa wamewekwa chini ya ulinzi. |
Operesheni kimbunga! Ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania ya kukomesha ujambazi na kukamata wahamiaji haramu, imeanza kwa waliokaidi mwito wa kuondoka nchini kwa hiari yao.
Operesheni hiyo ni ile iliyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete, aliposema majambazi na wahamiaji haramu, watasakwa misituni, majumbani na hata ardhi itachimbuliwa, kutafuta silaha walizozifukia.
Mkuu wa Operesheni za Polisi nchini, Simon Sirro, ambaye pia na Mkuu Msaidizi wa operesheni hiyo, amesema hayo jana alipozungumza na vyombo vya habari.
Mpaka sasa kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, aliyekuwepo katika mkutano huo, ni wahamiaji haramu 11,601 tu walioondoka wakati uongozi wa mkoa huo, ulitarajia wahamiaji haramu kati ya 52,000 na 53,000 waondoke.
Kamanda Sirro alisema tangu operesheni hiyo ianze juzi, wahamiaji haramu 1,851 wamekamatwa, ng’ombe 1,763 na silaha za moto saba, bunduki za kienyeji maarufu magobori sita na shotgun moja katika mikoa lengwa ya Kagera, Kigoma na Geita.
Katika Mkoa wa Kigoma, operesheni hiyo imefanikiwa kukamata wahamiaji haramu 885, silaha mbili, gobori moja na shotgun moja na ng’ombe 200.
Mkoani Geita, wahamiaji haramu 246 wamekamatwa, magobori matatu, ng’ombe 240, sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kibuyu cha maji cha jeshi hilo. Katika mkoa wa Kagera, wamekamata wahamiaji haramu 750, magobori mawili na ng’ombe 1,323.
Mbali na silaha hizo zilizokamatwa, silaha zingine 65 zimesalimishwa; SMG 3, shotgun 10 na magobori 52.
Kwa mujibu wa Kamanda Sirro, silaha nyingi zilisalimishwa katika wilaya ya Biharamulo na ndizo zilizokuwa zikitumika katika utekaji na unyang’anyi katika mapori wilayani humo.
Aliwataka wahamiaji hao na majambazi, kuendelea kusalimisha silaha zao na wakishindwa kuzikabidhi kwa vyombo vya dola, wazitelekeze popote na askari watafika na kuzichukua.
Alionya kuwa Jeshi halina mchezo hata kidogo katika operesheni hiyo, na yeyote atakayejaribu kujibizana nao wakiwa kazini, hawatasita kumwajibisha.
Kuhusu wahamiaji haramu walioolewa na Watanzania, Massawe aliwataka wafike katika ofisi za Uhamiaji, wapewe hati ya utambulisho zitakazotumika kwa muda wa miaka miwili, wakati wakisubiri utaratibu za kupata uraia.
Kwa wanawake walioolewa na Watanzania ambao waliondoka nchini kwa kutoelewa sheria, Massawe aliwataka warejee na kufika ofisi za Uhamiaji kupata hati za muda za kuishi nchini.
Alisema lengo la operesheni hiyo, si kutenganisha familia za wanandoa na watoto wao, kwa kuwa haki za binadamu zimezingatiwa.
Kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo, Rais Kikwete aliamuru majambazi na wahamiaji haramu wote katika mikoa hiyo lengwa, wajisalimishe katika muda wa siku 14 kuanzia Julai 26, mwaka huu.
Aliwataka wajisalimishe wenyewe ndani ya siku hizo 14, zilizomalizika Agosti 8, mwaka huu, kabla ya kuanza kwa operesheni kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania, yenye lengo la kukomesha ujambazi katika mikoa hiyo na kukamata wahamiaji haramu.
Rais katika agizo hilo, alielezea sababu ya Tanzania kufikia uamuzi huo kwamba ni kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukiukaji wa sheria na kuhatarisha amani kwa Watanzania, kunakosababishwa na wahamiaji hao na kuzagaa kwa silaha.
“Majambazi wanateka magari, wanaua watu wetu, wanapora mali zao. Watanzania hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu, woga na taabu katika nchi yao wenyewe. Tutawasaka majambazi misituni, tutawasaka majumbani, tutachimbua ardhini kutafuta hata silaha zilizofukiwa chini.
“Tumeamua kukomesha upuuzi huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita. Leo (Julai 26, mwaka huu) nimetoa maagizo kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Usalama wa Taifa, kuandaa operesheni maalumu, operesheni kubwa kuliko zote tangu tupate Uhuru. Upuuzi huu hauwezi kuendelea,” alisema Rais Kikwete.
Baada ya kumalizika kwa muda wa siku 14, baadhi ya wahamiaji haramu, ambao sasa ni 11,601 walitii agizo la Rais la kuwataka kujisalimisha na kurejea makwao.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alikutana na waandishi wa habari na kusisitiza mwito wa Serikali, kuwataka wahamiaji haramu hao waondoke wenyewe na mali zao bila kunyanga’nywa.
Aliwataka wenye mali nyingi, watoe taarifa katika vituo vya Polisi, ili wasindikizwe. “Hatutawavumilia wahamiaji haramu,” alisisitiza.
Kwa kutambua kuwa wako wahamiaji haramu hao, wanaopenda kuendelea kuishi nchini, Dk Nchimbi aliwataka wenye nia hiyo, kurudi nchini kwao kwanza na kufuata utaratibu wa kisheria kama ambavyo nchi nyingine zinavyofanya, wakati raia wa kigeni anapotaka kuishi katika nchi ambayo si ya uraia wake wa asili.
Hata hivyo, Dk Nchimbi aliwaonya wahamiaji haramu hao kuwa operesheni ya kuwaondoa katika mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa itaanza ghafla.
“Nimeshapewa maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete ya kuwaondoa wahamiaji haramu nitakapoona inafaa. Operesheni itaanza ghafla haiko mbali. Muda muafaka wa kutekeleza vyombo vya dola vitasema,” alisema.
Waziri alitoa onyo kwa viongozi wa vijiji wanaoshirikiana na wahamiaji hao kuwatunza na kusema jambo hilo ni makosa kisheria na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema pia kuna wahamiaji 14 wamerejea nchini tena bila kufuata utaratibu wa sheria, baada ya kurudi makwao na kuwataka wasilione jambo hilo kuwa ni mzaha.
Naye Massawe, ambaye ni miongoni mwa waongoza msako wa wahamiaji haramu, alisema jana kuwa wananchi wanao wajibu wa kuwafichua wahamiaji haramu na wamiliki wa silaha kinyemela.
Alisema kuna viongozi wamekuwa na tabia ya kuwaficha wahamiaji haramu badala ya kuwafichua na kuonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Alipiga marufuku mtindo ulioanzishwa na wahamiaji haramu, kuacha mali na vifaa vyao kwa baadhi ya wananchi, kwa makubaliano ya kurudi tena baada ya Operesheni Kimbunga kumalizika.
Aliwataka wahamiaji haramu waondoke na mali zao na kama hawawezi kuondoka nazo, waziuze kwa maandishi sio kuhifadhi kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment