Makao Makuu ya Chama cha Walimu Tanzania. |
Chama mbadala wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mtandao wa Walimu Tanzania (TTN), ambacho kimesajiliwa, kimeungwa mkono na Kamati ya Taifa ya Wanachama wa CWT.
Akizungumza na mwandishi Dar es Salaam jana, Katibu wa Kamati hiyo, Joseph Beda, alisema wameamua kuungana na TTN ambayo makao yake makuu ni Mwanza, ili kuunganisha nguvu katika kudai haki ya walimu wa shule za msingi, kujitoa CWT.
“Tumeona sisi kama Kamati, hatuwezi kupambana na uongozi wa CWT kwa kuwa hatutambuliki rasmi, lakini TTN ni chama halali chenye usajili na malengo yake ni sawa na sisi na Mwanza ina takribani walimu 800 wa shule za msingi wanaotaka kujitoa CWT kutokana na matatizo yaliyopo,” alisema Beda.
Tayari kamati hiyo na TTN wamekutana katika mkutano wao wa kwanza uliofanyika juzi, na kupitisha maazimio, ikiwemo kuanza kampeni ya kuhamasisha walimu wa shule za msingi, kujitoa CWT na kusimamisha makato ya michango yao kwa chama hicho, ambayo ni asilimia mbili ya mishahara yao kila mwezi.
Azimio lingine ni kuukataa kwa nguvu mgomo uliopangwa na viongozi wa CWT, unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, kwa kuwa wameona hauna tija na wala haulengi matatizo halisi ya walimu likiwamo la mishahara midogo.
“Tunachotaka ni sisi walimu wa shule za msingi, tuwe na nafasi kwenye chama hiki. Kwanza sisi ndio wengi na michango asilimia 75 na zaidi, ni ya walimu wa shule za msingi.
“Kama hatusikilizwi tunajitoa CWT na kuunda chama chetu, lakini hata tukijitoa, lazima tudai haki zetu za michango tuliyokatwa huko nyuma,” alisisitiza.
Alisema kwa sasa ndani ya chama hicho, hakuna usawa, nafasi nyingi kuanzia makao makuu ya chama hicho hadi wilayani, zinatolewa huku walimu wa shule za msingi wakiachwa jambo ambalo si haki, kwa kuwa wapo walimu wengi wenye uwezo, sifa na elimu.
“Bado kikao chetu hatujakimaliza... kuna mambo mengi hatujafikia uamuzi kama vile masuala ya CWT na biashara, mapato na matumizi ya chama na suala la Katiba, ambalo kwa sasa liko mahakamani, ila tunatarajia kukutana tena keshokutwa (Alhamisi) kumalizia majadiliano yetu,” alisema Beda.
No comments:
Post a Comment