ARIEL CASTRO AKUTWA AMEJINYONGA NDANI YA GEREZA...

Ariel Castro akisubiria hukumu yake mahakamani.
Mwanaume ambaye aliwashikilia mateka wanawake watatu nyumbani kwake kwa karibu miaka kumi kabla ya mmoja wao kutoroka na kuzitaarifu mamlaka husika amekutwa amekufa na inaaminika kuwa amejiua, maofisa wa gereza walisema.

Ariel Castro, mwenye miaka 53, alikutwa akining'inia katika selo yake usiku wa kuamkia leo katika kituo cha kurekebisha tabia huko Orient, kusini mwa Columbus katikati ya mji wa Ohio, JoEllen Smith, msemaji wa Idara ya Ukarabati na Urekebishaji, alisema asubuhi hii.
Mfanyakazi wa tiba katika gereza hilo alifanya huduma ya awali kabla ya Castro kupelekwa hospitali, ambako alitangazwa kufariki dunia muda mfupi baadaye.
Alikuwa kwenye uangalizi madhubuti sababu ya kuvuma kwa ubaya kesi yake, ikimaanisha alikuwa akiangaliwa kila baada ya dakika 30, lakini hakuwa akitazamwa kwa mazingira ya kujiua, alisema Smith. Alisema kutazwamwa kwa mazingira ya kujiua kunalazimisha uangalizi wa siku zote.
Castro alikuwa akitazamwa kwa karibu katika Gereza la Cuyahoga County katika wiki kadhaa baada ya kukamatwa kwake na kabla ya kesi yake kuamualiwa kwamba ana hatia, huku vifaa vikifuatilia vitendo vyake kila baada ya dakika 10. Alitolewa kwenye gereza hilo mapema Juni baada ya mamlaka kujiridhisha hakuwa kwenye hatari ya kujiua.
Wanasheria wa Castro walijaribu bila mafanikio kumfanyia uchunguzi wa akili katika Gereza la Cuyahoga County, ambako Castro alikuwamo kabla ya kupelekwa kwa mamlaka za jimbo hilo kufuatia kutiwa hatiani kwake, mwanasheria wake, Jaye Schlachet alieleza mapema leo. Schlachet alisema hawezi kueleza chochote zaidi kwa wakati huo.
Wanawake hao watatu walitoweka kwa wakati tofauti kati ya mwaka 2002 na 2004, wakati walipokuwa na umri wa miaka 14, 16 na 20. Walitoroka kutoka nyumbani kwa Castro Mei 6, pale Amanda Berry, mmoja wa wanawake hao, alipovunja sehemu ya mlango mmoja na kukimbilia kwa majirani kuomba msaada.
"Nisaidieni," alisema alipokuwa akipiga simu polisi. "Nimetekwa, na nilitoweka kwa miaka 10 na niko hapa, niko huru sasa."
Wanawake wengine wawili walikuwa na hofu mno ya Castro kiasi wakaendelea kushikiliwa mwanzoni hata pale polisi walipoanza kuzingira nyumba hiyo. Lakini haraka wakagundua kwamba wako huru.
"Mmetuokoa! Mmetuokoa!" mateka mwingine, Michelle Knight, alimweleza ofisa mmoja huku akijitupa mikononi mwake.
Castro alikamatwa jioni ya siku hiyo. Alikuwa pia akimlea mtoto mmoja aliyezaa na Berry wakati akiwa mateka; binti huyo alikuwa na umri wa miaka 6 wakati alipoachiwa huru. Jaji mmoja alikataa maombi ya Castro kupewa haki za kumtembelea binti yake huyo.
Castro alihukumiwa kifungo cha maisha jela Agosti 1 pamoja na miaka 1,000 kwa kupatikana kwake na hatia katika mashitaka 937 ikiwamo utekaji nyara na kubaka.
Katika taarifa ya kutapatapa, alimweleza jaji huyo hakuwa dubwana ila mtu mwenye maradhi ya kutawaliwa na ngono.
"Mimi sio dubwana. Ninaumwa," alisema Castro wakati wa hukumu yake.
Knight alikuwa pekee kati ya wanawake hao watatu aliyehudhuria mahakamani wakati wa hukumu yake.
"Umepoteza miaka 11 ya maisha yangu, na nimerejea," alisema kwenye chumba cha mahakama. "Nimetumikia miaka 11 kuzimu. Sasa jehanamu yako ndio kwanza inaanza."
Hili ni tukio la pili kubwa kwenye gereza la Ohio katika kipindi cha mwezi mmoja.
Agosti 4, mfungwa aliyekuwa akisubiria utekelezwaji wa adhabu yake ya kifo alikuwa amejinyonga ndani ya selo yake siku chache tu kabla ya kuuawa. Alikuwa akishutumiwa kwa mauaji ya kutisha ya jirani yake kwa kumchoma visu.

No comments: