Monday, August 5, 2013

WASICHANA WA SHULE WAISHI KWA HOFU YA KUBAKWA SUMBAWANGA...

Bweni la wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bomalang'ombe iliyoko wilayani Kilolo, mkoa wa Iringa. Ukosefu wa mabweni madhubuti kumekuwa kukichangia vitendo vya kubakwa kwa wanafunzi wa kike.
Wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Mzindakaya kijijini Kaengesa, wameelezea vitendo hatari wanavyokabiliwa navyo vya kubakwa na kudhalilishwa kijinsia mara kwa mara, kutokana na kukosa uwezo wa kuishi katika mabweni kwa usalama.

Wakizungumza na mwandishi katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki, wanafunzi hao wamedai kuwa wamekuwa wakiona aibu kuripoti visa vya ubakaji  wanavyofanyiwa, kwa uongozi wa shule na kwa wazazi  wao.
“Wengi wetu hatujui hatima yetu kwani tunaishi kwa hofu  kubwa hususani usiku, tunakosa  raha  licha  ya kwamba  kila mmoja  wetu amepanga chumba.
“Kutokana na visa  vya kubakwa  mara  kwa mara, tumeamua  kulala  chumba kimoja  wasichana  kati  ya  watatu hadi  sita,” alisema mmoja wao.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, wamekuwa wakiogopa na kuona aibu  kutoa taarifa kwa mamlaka husika, na kubakia kukaa kimya na  kujiuguza kwa siri na hata wakipiga kelele, huwa hawapati msaada.
“Tukipiga kelele, hakuna msaada mpaka kukicha ndipo majirani wanapokuja kutupa pole huku wakidai  kuwa licha ya kusikia tukipiga  mayowe  ya kuomba msaada,  wanashindwa kutoka  nje  kwa hofu ya  kushambuliwa  na watu hao wasiojulikana,“ alisema mmoja  wa wanafunzi hao kwa masikitiko.
Akizungumza  na mwandishi shuleni hapo  hivi  karibuni, Makamu Mkuu wa shule  hiyo, Agatha Okumu, alikiri  kuzungumza na  wanafunzi wa kike wanaoishi katika  nyumba za kupanga kijijini, wakamweleza kuwa kumekuwa na visa vingi vya  kubakwa. 
 “Nyumba  walizopanga  hazifai  kuishi, hazina  usalama kutokana na  milango  ya  vyumba kuwa mibovu na usiku wanalazimika  kuegesha vinu kuzuia  isifunguke.
“Sasa imekuwa rahisi kwa ‘wabakaji‘ kusukuma tu milango  hiyo na kuingia  ndani  na kuwaingilia kimwili na kutokomea  kusikojulikana,“ alisema.
Alisema visa  vya kubakwa  wanafunzi  hao  wa kike   ni  vingi, lakini  vitatu tu ndio vimeripotiwa  hadi  sasa  ambapo  kisa  cha  kwanza kiliripotiwa  baada ya wanafunzi  watatu  kubakwa,  na mtuhumiwa  alisakwa na kukamatwa na kufikishwa katika  vyombo  vya dola.
Kwa mujibu wa Mwalimu Okumu, visa vingine  ni  pamoja  na  mwanafunzi  wa kidato  cha nne  shuleni  hapo, aliyejiua  kwa kunywa sumu  ya panya,  baada  ya  kubakwa  yeye na  mwenzake mwingine.
Mtu aliyewafanyia hivyo, kwa maelezo ya Mwalimu Okumu, alivamia chumbani mwao walimokuwa wakiishi watatu  na kuwatishia  kuwaua iwapo  wangepiga  kelele.
“Juzi  tu wanafunzi sita waliokuwa wakiishi chumba kimoja wamenusurika kubakwa na  watu  wawili  waliowavamia usiku wakiwa wamelala  chumbani mwao.
“Hata hivyo walishindwa kuwafanyia  vitendo  vya udhalilishaji baada ya  kukuta ni wengi  na  walianza kupiga mayowe, wakaishia kuwapora Sh 1,100 walizokuwa nazo, wakawapiga kwa marungu  na kutokomea  kusikojulikana,“  alisema Mwalimu Okumu.
Mkuu  wa shule hiyo,  Nicholas Thomas  amewatupia lawama majirani  wanaoishi karibu na  nyumba walizopanga wanafunzi  hao, kwa kutowapatia  msaada wowote  licha ya  wao kupiga mayowe  ya kuomba  msaada.
Mwalimu Thomas aliwataka wazazi kuchangia  gharama za  watoto  wao  kuishi katika mabweni  shuleni  hapo,  ambapo  kwa mtoto  mmoja kwa muhula,  mzazi anatakiwa  kuchangia  magunia  mawili  ya mahindi, debe moja la  maharage na Sh 40,000 za  ujira  wa mpishi.
Umasikini wa wazazi wao, umedaiwa kusababisha wanafunzi hao kushindwa kulipia gharama za kuishi katika mabweni ya shule hiyo, na kwa kuwa wanahitaji elimu, wakalazimika kupanga nyumba mbovu, ambazo ndizo hufanyiwa vitendo hivyo.
Mwandishi alipotembelea baadhi ya nyumba walizopanga  wanafunzi hao na kushuhudia zikiwa katika hali mbaya, kwani hazina vyoo na wala hazijazungushiwa uzio kwa ajili ya usalama wao.
“Kama  unavyoona choo kilichopo ni kibovu, hakina hata  mlango na kiko nje meta kadhaa kutoka katika nyumba hii. Kutokana na hofu ya kutoka nje kujisaidia wakati wa usiku, tunalazimika kujisaidia kwenye makopo tunayohifadhi vyumbani kisha  asubuhi tunaenda  kumwaga uchafu huo chooni,” alisema.
Uchunguzi wa mwandishi umebaini kuwa kodi ya pango ya vyumba hivyo ni Sh 1,000 kwa mwezi.

No comments: