VIWANJA 7,800 VINAMILIKIWA NA WAMILIKI HEWA...

Kabwe Zitto.

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imebaini kuwapo wamiliki hewa wa viwanja 7,800 nchini, ambavyo vimetolewa na kupewa hati. 

Kutokana na upungufu huo, Kamati hiyo imemwagiza    Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kupitia upya utoaji viwanja hivyo.
Mwenyekiti wa PAC, Kabwe Zitto alisema hayo jana, baada ya kukataa kupokea taarifa ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi.
Kwa mujibu wa Zitto, katika Jiji la Dar es Salaam peke yake, Kamati ilibaini viwanja 160, vyenye thamani ya Sh milioni 500, ambavyo wamiliki wao hawajulikani.
Upungufu huo kwa mujibu wa Zitto, ni moja ya sababu za Kamati hiyo, kukataa kupokea taarifa ya Wizara hiyo na kuwataka kufika mbele ya Kamati Januari mwakani baada ya kufanyia kazi marekebisho. 
Matatizo mengine yaliyojitokeza katika Wizara hiyo, ni  kutofikia malengo yaliyowekwa na Serikali kukusanya mapato.
Zitto alitolea mfano kiwango kilichowekwa katika Bajeti ya mwaka 2012/13, ambapo Sh bilioni 99 zilitarajiwa kukusanywa kutokana na kodi na uuzaji viwanja, lakini wizara ilikusanya Sh bilioni 20 pekee. 
“Baada ya kuona wameshindwa kufikia lengo, waliamua kupandisha kodi na bei za viwanja na kuwaongeza mzigo   wananchi,” alisema.
Alisema Kamati imeiagiza wizara hiyo itakaporejea, kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuanzisha mfumo wa utoaji hatimiliki za viwanja, utakaotolewa kwa njia ya kielektroniki zikiwa na Namba ya Mlipa Kodi (TIN).
“Tunajua utoaji upya wa hati unaweza kulalamikiwa na watu, lakini tunaamini kupitia mfumo huo ambao kila mmiliki atatambulika kupitia TIN, utawezesha kuondoa migogoro iliyopo sasa wa eneo moja kumilikiwa na watu wengi na Serikali kupata mapato yake,” alisema.
Katika hatua nyingine, Zitto alisema PAC imeagiza  Jeshi la Polisi kutoa maelezo ya kwa nini Kikosi chake cha Usalama Barabarani, hakitumii  mfumo wa digitali kutoa stakabadhi za malipo, zinazotokana na makosa ya barabarani na kuwataka kutoa hoja zao mbele ya Kamati hiyo Septemba 10.
“Ni muda sasa tangu mfumo huo uanzishwe na vifaa vya utekelezaji wa kazi hiyo vinunuliwe na Serikali, lakini hadi sasa askari wa usalama barabarani wamekuwa wakitumia mfumo wa zamani wa utoaji stakabadhi,” alisema.
Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ilitoa taarifa kuwa kama mfumo huo ungetumika, ungeingiza serikalini Sh bilioni 55, tofauti na mfumo wa sasa ambao unakusanya Sh bilioni 15 kwa mwaka.
Hata hivyo, alieleza kuwa tayari wamewasiliana na TRA kuangalia mfumo utakaowezesha kutolewa kwa gawio, ambalo litawezesha askari wa usalama barabarani wakati utekelezaji wa mfumo mpya utakapoanza.

No comments: