Shekhe Ponda Issa Ponda. |
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilihamia kwa muda katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI), ambapo Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda, alisomewa mashitaka ya kuhamasisha vurugu maeneo tofauti nchini.
Ponda aliyelazwa katika wodi maalumu hospitalini hapo, alisomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka, Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa.
Hata hivyo waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia ndani ya chumba hicho, agizo lililotolewa na askari Polisi.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, ambayo waandishi wa habari walipewa na Wakili wa Shekhe Ponda, Juma Nassoro, kiongozi huyo anadaiwa kutenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Juni 2 hadi Agosti 11 mwaka huu, katika maeneo ya Zanzibar, Dar es Salaam na Morogoro.
Akizungumza nje ya chumba cha muda cha Mahakama hospitalini hapo, Wakili Nassoro alidai kuwa watapinga mashitaka hayo, kwa kuwa baadhi ya siku zilizotajwa zina utata, ikiwemo Agosti 11 aliyodai kuwa siku hiyo Shekhe Ponda alikuwa amelazwa hospitalini akiuguza majeraha.
“Tumepanga kwenda kupinga mashitaka hayo siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo…ukiangalia hati ya mashitaka ina upungufu wa mambo mengi, na kwa bahati mbaya wakati akisomewa mashitaka hayo, sisi hatukuwepo ndani ya chumba hicho,” alidai Wakili Nassoro.
Kwa mujibu wa madai ya Wakili wa Ponda, kesi hiyo ilisomwa muda mfupi baada ya wao kutoka nje ya hospitali hiyo, kwa kudhani kama siku imepita.
Alidai pia mashitaka hayo yalisomwa kwa mteja wake, katika muda ambao saa za kazi zilikuwa zimekwisha, hatua aliyodai kuwa ni ukiukwaji wa sheria na wanajiandaa kutumia hoja hiyo pia kupinga mashitaka hayo mahakamani.
Hata hivyo baada ya mashitaka hayo kusomwa, Wakili Nassoro alidai aliwahi kuomba mteja wake asiondolewe hospitali hapo, kwa madai kuwa bado hali yake si nzuri mbali na maumivu aliyonayo katika eneo la bega la kulia.
Ulinzi katika eneo hilo ulikuwa wa kutosha, huku magari matano ya Polisi yaliyokuwa yamebeba askari wa kutuliza ghasia, yakiwa katika eneo hilo tayari kwa kulinda usalama. Pia kulikuwepo gari maalumu lililokuwa limeandaliwa tayari kumbeba Shekhe Ponda.
Zaidi ya wafuasi 100 walijitokeza hospitalini hapo wakati mahakama ikiendelea na shughuli zake, hali iliyosababisha msuguano wa hapa na pale na polisi waliokuwa wakizuia wafuasi hao kwenda kumsalimia kiongozi huyo.
Mmoja wa watu waliozuiwa na polisi alipofika kumuona Shekhe Ponda wakati kesi ikiendelea, ni wakili maarufu, Profesa Abdallah Safari.
Shekhe alilazwa Muhimbili baada ya kujeruhiwa bega la kulia inadaiwa katika jaribio la Polisi kutaka kumkamata mkoani Morogoro.
Hata hivyo uchunguzi wa wataalamu wa taasisi hiyo, alikolazwa Shekhe Ponda ambako alifanyiwa upasuaji upya, ulishindwa kubaini kilichomjeruhi.
“Kutokana na tiba ya awali aliyopewa, ikiwa ni pamoja na kushonwa jeraha kabla ya kufikishwa Moi, imekuwa vigumu kujua jeraha lilisababishwa na kitu gani,” taarifa ya taasisi hiyo ilieleza.
Mbali na kutojua kilichomjeruhi Ponda, Msemaji wa Moi, Jumaa Almasi, aliripotiwa akisema hali ya Shehe Ponda anaendelea vizuri, ikilinganishwa na alivyokuwa kabla ya kufikishwa hospitalini hapo Jumapili iliyopita.
No comments:
Post a Comment