BENJAMIN MKAPA 'AFAGILIA' UWEPO WA SHULE ZA SEKONDARI ZA KATA...

Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amepongeza uwepo wa sekondari za kata na kuitaka Serikali isibadili mitaala na vitabu vya kiada kila mara.

Amesema sekondari hizo zimesaidia kuongeza udahili wa wanafunzi na kutaka changamoto zilizopo zipewe muda wa kupatiwa ufumbuzi lakini mitaala na vitabu visibadilishwebadilishwe kwani kunachanganya walimu na wanafunzi.
Amesema iwapo mabadiliko hayo yatakuwa na ulazima basi kuwe na muda ili walimu waelewe mitaala inavyotumika, kwani kubadili vitabu hivyo mara kwa mara kunanufaisha watunzi na si wanafunzi.
Mkapa alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya shule ya sekondari ya Shaaban Robert na kusema mitaala inatakiwa kuwa na mwendelezo na si kuibadili.
Alisema masuala hayo hayahitaji muda mrefu kuboresha elimu nchini hususan katika sekondari za kata, kama ilivyo katika kupata uwiano wa walimu na wanafunzi, vyumba vya madarasa na maabara zanye vifaa.
 “Kubadilisha mara kwa mara kunachanganya walimu na wanafunzi, lakini ikiwa vitakuwapo na kupangwa na kukubalika na walimu wakielewa kutokana na mafunzo ya mitaala kutakuwa na ufundishaji na uelewa mzuri,” alisema Mkapa.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuliwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Andy Chande, alisema katika kuandhimisha miaka hiyo, walifanya matembezi ya hisani.
Akifafanua, alisema matembezi hayo yalilenga kuchangia elimu kwa kujenga visima katika shule tatu za Dar es Salaam na kupaka rangi katika wodi tatu za hospitali za wilaya.
Mkuu wa Shule hiyo, Suryakant Ramji, alisema siri ya walimu wa shule hiyo kukaa muda mrefu hadi miaka 40 ni kuwajali na kuwapa motisha.
Pia alitaka katika kubadilisha mitaala kuwe na mafunzo kwa walimu kila inapobadilika ili kuwajengea uwezo na kuwapa nyenzo za kufundishia.

No comments: