PACHA ALIYETENGANISHWA MUHIMBILI ASUBIRI KUTENGENEZEWA NJIA YA HAJA KUBWA...

Madaktari wakifanya upasuaji katika Hospitali ya Muhimbili.
Saa 24 mara baada ya upasuaji wa kuwatenganisha watoto mapacha waliokuwa wameungana uliofanywa na jopo la madaktari bingwa saba, kutoka Hospitali ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu na Mifupa (MOI), Dar es Salaam, mtoto mlengwa wa upasuaji huo ameonesha maendeleo mazuri na sasa ameanza kunyonya bila ya usumbufu.

Upasuaji huo ulifanyika juzi MOI ukitumia saa 4 kwa kuwatenganisha mapacha hao waliokuwa wameungana sehemu ya mgongoni na miguuni, huku mmoja hakuwa amekamilika kimaumbile, jambo lililowalizimu madaktari kuwatenganisha kwa lengo la kumnusuru mmoja aliyekamilika.
Madaktari waliofanikisha upasuaji huo ni pamoja na Dk Robert Mhina ambaye ni mtaalamu wa mifupa, Profesa Karim Manji, mtaalamu wa mapigo ya moyo, Dk Hamis Shaaban, mtaalamu wa ubongo na uti wa mgongo na Dk Karima Khalid mtaalamu wa dawa ya usingizi.
Wengine ni Dk Zaitun Bokhary, bingwa upasuaji watoto na Dk Nyangasa mtaalamu wa moyo na mishipa ya fahamu na Dk. Petronila Ngiloi bingwa wa watoto ambaye ni mstaafu katika hospitali hiyo aliyeitwa kwa ajili ya kusaidiana na madaktari wenzake kufanikisha upasuaji huo.
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu maendeleo ya kichanga huyo, mmoja wa madaktari waliofanikisha upasuaji huo Dk Zaitun Bokhary, alisema kwa saa 24 tangu upasuaji huo ufanyike zimewapa matumaini kutokana na mtoto huyo kuendelea vizuri kiasi cha kumfanya kuwa na uwezo wa kunyonya.
“Nilikuwa nikifuatilia maendeleo yake usiku kucha saa chache tangu tulipomfanyia upasuaji, ukweli anaendelea vizuri ni mchangamfu na wakati wowote kuanzia sasa nitatoa ruhusa ya kumrejesha wodini kutoka ICU (chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu),” alisema Dk Bokhary.
Huku akionesha furaha yake kuhusu maendeleo ya mtoto huyo, Dk Bokhary alisema anajihisi kuwa ni mwenye furaha kubwa kutokana na maendeleo ya mtoto huo aliyewafanya waumize kichwa kwa siku kadhaa tangu alipofikishwa hospitalini hapo.
“Alisema kufanikiwa  kwa upasuaji huo kunapaswa kuleta fikra mpya kwa Watanzania kuwa hospitali zetu zina uwezo katika kufanikisha upasuaji wowote kutokana na uwepo wa wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa.
Alisema si jambo la busara kukimbilia katika hospitali zilizopo nje ya nchi na kupoteza fedha nyingi pasipo sababu yoyote kwa kuwa tiba na upasuaji wa kila aina kwa sasa unawezekana hapa nchini.
Alisema upasuaji wa mtoto huyo umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 95 na kwamba asilimia tano zilizobakia zimetokana na kutomfanyia upasuaji wa sehemu ya haja kubwa baada ya hali ya mtoto kuonekana kubadilika walipokuwa wakiendelea na upasuaji huo mdogo wakati wakisubiri kumfanyia upasuaji mwingine ndani ya miezi mitatu ijayo kwa ajili ya kupata sehemu ya haja kubwa.

No comments: