Mmoja wa askari wa zimamoto akizima moja ya mitambo hiyo jana asubuhi. |
Moto mkubwa uliozuka katika mitambo ya kuzalisha umeme ya Songas Ubungo, Dar es Salaam, umeathiri mitambo na vifaa vya umeme na kusababisha baadhi ya maeneo ya Jiji hilo, kukosa umeme, hali inayotarajiwa kuchukua zaidi ya wiki.
Maeneo hayo kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felchesmi Mramba, yatahusu wilaya za Ilala na Kinondoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alitaja maeneo yatakayoathirika kuwa ni Magomeni, Tandale, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Changanyikeni, Kimara, Mbezi, Tabata na Ubungo River Side.
Akisimulia ajali hiyo, Mramba alisema ulizuka saa 9.45 alfajiri na kuunguza nyaya za kusafirishia umeme kutoka mitambo hiyo, hali iliyosababisha Jiji la Dar es Salaam kukosa umeme kuanzia saa 10 alfajiri.
Alisema baada ya moto huo ambao hadi sasa chanzo chake hakijafahamika, askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Jiji kwa kushirikiana na kikosi cha wazimamoto na waokoaji binafsi wa Night Support, walifanikiwa kuuzima kabla haujasambaa kwenye mitambo mingine.
“Hadi sasa hatujabaini chanzo cha moto huu na uchunguzi unaendelea, tunachoweza kusema sasa ni tunachokiona kwa macho, kwamba kuna nyaya zimeungua… baada ya uchunguzi kukamilika tutatoa taarifa,” alisisitiza Mramba.
Pamoja na kuungua kwa nyaya hizo, alisema baadhi ya vifaa kwenye vituo vidogo vya umeme pia vimeungua na shirika litatoa taarifa kamili ya mali zilizoharibiwa na moto huo, uchunguzi ukikamilika.
Alisema shirika kwa sasa linajitahidi kuhakikisha hali katika eneo hilo, inarejea kawaida kwa kuanza na uhakiki wa ukubwa wa tatizo na kuangalia vifaa vilivyoharibika ambavyo vinahitaji kurudishwa upya ikiwamo nyaya kutandazwa upya.
Alitumia fursa hiyo kuomba radhi wananchi kutokana na usumbufu unaojitokeza kwa tukio hilo na kuwataka watoe ushirikiano kwa shirika ili umeme uweze kurudi haraka.
Kuhusu muda wa huduma za umeme kurejea katika maeneo yaliyoathiriwa na moto huo, Mramba alisema kwa uhakiki wa haraka kazi hiyo inatarajiwa kukamilika baada ya wiki kadhaa.
"Hii si kazi ya saa kadhaa au siku moja, mafundi watakapoanza kazi tutajua vitu vilivyoungua na vinakopatikana na tutakachokifanya ni kuangalia namna ya kuwapa watu umeme kutoka vituo vingine," alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, aliyetembelea mitambo hiyo baada ya kupata taarifa za moto, aliagiza shirika hilo kuhakikisha uchunguzi wa haraka unafanyika na kutoa taarifa kuhusu sababu za moto huo.
“Lakini pia katika maeneo ambayo yataathiriwa kwa kukosa umeme, jitihada zifanyike ili warejeshewe waendelee na shughuli zao za kawaida,” alisisitiza.
Kwa upande wa Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jesuald Ikonko, alisema kikosi chake kilipokea taarifa za kuungua mitambo hiyo saa 11.58 alfajiri na walifika eneo la tukio saa 12.05 asubuhi.
Alibainisha kuwa kikosi hicho kilichelewa kufika eneo la tukio kutokana na taarifa za kuungua kwa mitambo hiyo kuchelewa kuwafikia, kwani moto ulianza saa 9.45 alfajiri lakini kikosi hicho kikataarifiwa saa 11.58.
“Kikosi hiki kinafanya kazi saa 24 na kina askari na vifaa vya kutosha, ni vizuri matukio ya ajali yanavyotokea tupewe taarifa mapema ili tufike mapema kwenye maeneo hayo na kufanya kazi ya uokoaji haraka,” alisisitiza.
Alitaka wananchi waache kisingizio kwamba namba zao hazipatikani, kwani wana namba zaidi ya tatu na zote zinafanya kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alishukuru wafanyakazi wa Tanesco na vikosi vya ukoaji kwa jitihada walizoonesha katika uzimaji moto na kuomba wananchi wavute subira katika kipindi ambacho hawatakuwa na umeme.
No comments:
Post a Comment