Biblia Takatifu. |
Bila yeye mwenyewe kutarajia, mke wa ndoa amejikuta akicharazwa bakora na kutimuliwa nyumbani na mumewe baada ya mama huyo kuacha kuabudu katika madhehebu ya Katoliki alikofunga ndoa na mumewe aitwaye Martin Kikondo (50) na kuamua kubatizwa na kuanza kusali katika Kanisa la Assemblies (EAGT).
Mama huyo aitwaye Redempta Saulo (38) mkazi wa kijiji cha Kasokola wilayani Mlele, mkoani Katavi alikumbwa na dhahama hiyo hivi karibuni baada ya yeye na watoto wake watatu 'kuasi’ Kanisa Katoliki na kuanza kusali katika kanisa hilo la EAGT bila idhini ya mumewe huyo.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kasolola, Dominico Fungameza akisimulia mkasa huo alieleza kuwa wanandoa hao walitengana hivi karibuni mwanzoni mwa wiki iliyopita baada ya Martin kubaini kuwa mkewe na watoto wake watatu wamebadili madhehebu bila kumshirikisha.
Alisema mume huyo baada ya kugundua kuwa mkewe amebadili dhehebu lake la awali pamoja na watoto wake bila ridhaa yake alihamaki na kuanza kumpiga mkewe huyo ambaye alikimbilia Kituo cha Polisi ili kujisalimisha na baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya mjini hapa kwa matibabu.
“Hata hivyo Polisi waliwashauri wanandoa hao wamalize mgogoro wao kifamilia … lakini ushauri huo ulipingwa na viongozi wa kiroho wa kanisa hilo la EAGT,” alisema Fungameza.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, Mchungaji wa kanisa hilo aliyemtaja kama Jacob Mizengo alilazimika kumfuata Martin nyumbani kwake ambako alihoji kulikoni amechukua uamuzi wa kumpiga mkewe kisa amejiunga na kanisa la EAGT.
Inadaiwa ndipo Martin na mchungaji huyo kuanza kutupiana maneno ya kutishiana na kusababisha zogo lililofanya majirani kusogea nyumbani hapo ili kujua kilichokuwa kikiendelea akiwemo mwenyekiti wa kijiji hicho katika jitihada za kuwasuluhisha.
Ndipo majirani hao waliokusanyika nyumbani kwa wanandoa hao waliamua kifanyike kikao cha usuluhishi kilichowahusisha baadhi ya wazee na wanandugu wa pande hizo mbili za mwanandoa hao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Fungameza.
Hata hivyo wakati kikao hicho kikiendelea ndipo Martin aliingia ndani ya nyumba yake na kisha alitoka akiwa ameshikilia picha ambazo alizionesha mbele ya wajumbe wa kikao hicho jinsi mkewe na watoto wake walivyo kuwa wakibatizwa na Mchungaji Mizengo, ubatizo ambao uliofanyika mtoni kijijini Kasokola.
Inadaiwa kuwa baada ya kuwaonesha picha hizo mbele ya wajumbe wa kikao hicho wakiwemo ndugu zake , Martin aliwaeeleza kuwa yeye hayuko tayari tena kuendelea kuishi na mkewe huyo kwa kuwa amebadili dhehebu hivyo hataki kumwona nyumbani kwake tena.
Kufuatia msimamo huo wa Martin mbele ya kikao hicho kwa kuhofia usalama wa wanandoa hao kikao hicho kiliridhia kuwa mke wa Martin aende akaishi nyumbani kwa wazazi wake kijijini humo mpaka hapo watakapo suluhishwa na ndugu zao wa pande hizo mbili.
No comments:
Post a Comment