Dk John Magufuli. |
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, amesema Serikali haitasita kubomoa nyumba za wananchi waliosusia kuchukua fedha za fidia za nyumba zao, ili miradi ya ujenzi iendelee bila kuchelewa.
“Sasa naagiza hawa watu wanane wa hapa Kigamboni kwanza nipatiwe majina yao, lakini pia nataka wajiandae ama kukubali kulipwa fidia au wabomolewe mradi uendelee,” alisema Magufuli.
Alisema hayo Dar es Salaam jana, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya Dar es Salaam, ikiwemo ujenzi wa daraja la Kigamboni.
Miradi mingine aliyokagua ni pamoja na barabara ya
Yombo Vituka-Devis Kona, Kigogo-Jangwani, Morocco-Mwenge, Mradi wa Mabasi ya Kasi (Dart), eneo la Mwembe Chai, Ubungo, Jangwani na Kivukoni.
Aliwageukia wananchi wanaokwamisha miradi
ya ujenzi, kwa kukubali kulipwa fidia na baadaye kugeuka na kukimbilia mahakamani, kuwa hasara itakuwa yao.
Aliwatahadharisha kuwa endapo Serikali itashinda kesi hizo, nao watashitakiwa na kulipa hasara iliyotokana na miradi hiyo kucheleweshwa.
Tayari fedha za fidia katika mradi wa daraja la Kigamboni, zimeshatengwa na kati ya wananchi 121 waliostahili kulipwa fidia hizo, 113 wamekubali kufanyiwa tathmini na kupokea malipo ya Sh bilioni 11.7, isipokuwa wananchi hao wanane ambao wamegoma kupokea fidia hizo.
Alisisitiza kuwa kwa sasa Serikali haiko tayari kuona baadhi ya watu wanachelewesha kwa makusudi miradi ya maendeleo, huku akitoa mfano wa mradi wa Kigamboni ambao utagharimu Sh bilioni 214, kati ya fedha hizo asilimia 60 zimetolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Akitoa taarifa ya maendeleo ya daraja la Kigamboni, Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa NSSF, Karim Mataka, alisema hadi sasa awamu ya kwanza ya ujenzi huo ambayo ni kuweka na kujengea nguzo za chuma zaidi ya 200, imefikia asilimia 47.
Akikagua ujenzi wa barabara ya Kigogo-Jangwani, ambako kuna mkandarasi anayejenga barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 2.7, Hari-Singh kwa gharama ya Sh bilioni 7.6, Magufuli, alisikitishwa na taarifa kwamba kampuni hiyo imesitisha ujenzi kwa miaka mitatu sasa, kutokana na baadhi ya wananchi waliolipwa fidia, kukata rufaa na kwenda mahakamani.
“Huu ni mwaka wa tatu sasa tupo tu hapa, zipo nyumba 13 zilizopimwa na kufanyiwa tathmini ya Sh bilioni 3.8, lakini cha kushangaza kati ya nyumba hizo sita, wamiliki wake baadaye walidai fedha hizo ni ndogo na kugoma kuondoka na mwishowe walikimbilia mahakamani,” alisema Musa Ally ambaye ni mshauri wa mradi huo.
Akizungumzia suala hilo, Magufuli alimuagiza mkandarasi wa mradi huo uliotakiwa kukamilika rasmi tangu Oktoba mwaka 2010, kuendelea kujenga na kupitisha barabara hiyo kuzizunguka nyumba ambazo wamiliki wake wamefungua kesi mahakamani.
“Nakuagiza endelea na ujenzi, haiwezekani mkandarasi ukae tu bure kwa miaka mitatu halafu baadaye Serikali ije kuingia gharama ya kukulipa, nawaagiza Wakala wa Barabara (Tanroads), nanyi mjiandae kufungua kesi dhidi ya wananchi hawa, tukishinda kesi wao ndio walipe mzigo wa hasara hii ya kuchelewa kukamilika kwa mradi,” alisema Magufuli.
Akikagua ujenzi wa barabara ya Yombo Vituka-Devis Kona ya urefu wa kilometa 10.3, alitaarifiwa kwamba wananchi waliotathminiwa na kulipwa fidia ya Sh bilioni 15.8, ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo, hadi sasa wamegoma kuondoka na wengine kukimbilia mahakamani.
“Sheria iko wazi kwamba mtu ukishalipwa fidia yako halali kabisa, unatakiwa upishe eneo husika ndani ya siku 90, sasa naagiza, ambao mmeshawalipa na bado wanasuasua kuondoka, bomoeni muendelee na ujenzi,” alisisitiza.
Kuhusu mradi wa Dart, ambao awamu ya kwanza unagharimu kiasi cha Sh bilioni 288, Magufuli alipongeza hatua iliyofikiwa, lakini aliagiza uchunguzi wa haraka ufanyike ili kubaini wanaoharibu miundombinu ya mradi huo kabla haujakamilika.
Magufuli alitoa agizo hilo, baada ya kutaarifiwa na Meneja wa Mradi Dart kutoka Tanroads,Barakaeli Mlay, kuwa pamoja na mradi huo kufikia takribani asilimia 60, lakini changamoto kubwa ni wananchi wanaofungulia maji ya vyooni kwenye mifereji ya maji ya mvua.
“Si hivyo tu hapa jioni utakuta watu wamejazana wanafanya biashara zao, wenye bodaboda wanaangalia maeneo ambayo sisi tumejenga maalumu kwa ajili ya kupitishia maji wakati wa mvua, wao wanapita na kubomoa. Hii ni hasara ambayo baadaye itabidi Serikali ilipe,” alisema.
Kutokana na taarifa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alimtaka mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Strabag kutoka Ujerumani, kuripoti matukio yote ya wananchi yanayochangia kuharibu mradi huo, ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kulipa hasara watakayoisababisha.
No comments:
Post a Comment