Friday, July 26, 2013

WAGANGA WA KIENYEJI SAUZI WAMTAMBIKIA MZEE MANDELA...

Hospitali alikolazwa Mzee Mandela mjini Pretoria.
Kundi la waganga wa kienyeji kutoka mkoa wa Gauteng, wameamua kutambika nje ya hospitali aliyolazwa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Waganga hao juzi walichoma ubani kwenye kibuyu, wakasujudu huku wengine wakinyunyiza unga wa tumbaku na kuimba, ili kuita mizimu ya Madiba, ije kumponya.
Kiongozi wa Baraza la muda la waganga hao, Khubane Mashele, aliomba mizimu ya waliokufa wakati wa mapambano ya kudai uhuru, isaidie kumponyesha kiongozi huyo, shujaa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
"Tumeiita mizimu ya wafalme na askari waliopigana wakati wa mapambano ya kudai uhuru, itusaidie kuita mizimu ya mababu wa Mandela, ili isaidie kumponya kwa kuwa bado tunamhitaji,” Mashale alisema wakati wa tambiko hilo.
Kabla waganga wengine kutoka Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, waliwasili katika hospitali hiyo ya Medi-Clinic, kufikisha ujumbe wa matumaini ukiambatana na ndoo iliyokuwa imepambwa maua. 
Mwenyekiti wa waganga hao kutoka Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini, Kgosi Madoda Zibi, alisema ujumbe huo ulilenga kufikishwa kwa familia ya Mandela.
"Tumepewa mamlaka na waganga wa Kaskazini Magharibi kuja kufikisha ujumbe wa matumaini,” alisema Zibi.
"Kwa ujumbe huu, tunamshukuru Mandela kwa mchango wake katika ukombozi wa nchi yake.”
Zibi na ujumbe wake, walielekezwa kuweka maua hayo na kadi za kumtakia Mandela heri katika ukuta nje ya hospitali hiyo, eneo maalumu kwa ajili ya kuweka ujumbe wa kumtakia heri Mandela.
Hivi karibuni wakati wa sherehe ya miaka 95 ya Mandela, binti yake, Zindzi, alisema kwa sasa kiongozi huyo anaweza kuangalia televisheni na hata kunyanyua mkono.
Alisema shujaa huyo anaweza kuruhusiwa hivi karibuni, kwani alipomtembelea alikuwa akiangalia televisheni huku akiwa anatumia spika za masikioni, alitoa tabasamu zuri na kuitika kwa macho.
Alisema baba yeke amekuwa akipata nguvu kadri siku zinavyokwenda na anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani wakati wowote.

No comments: