![]() |
| Anna na mumewe, Phil wakiwa wamempakata mtoto wao 'wa miujiza', Esme. |
Huyu ni mtoto wa miujiza - aliyezaliwa baada ya miaka 10 na mara 10 za matibabu ya utungishaji mimba.
Esme Binks alizaliwa miezi mitano iliyopita baada ya mapambano ya muda mrefu ambayo yalimgharimu mama yake, Anna mpepesuko wa kiasi cha Pauni za Uingereza 35,000.
Anna, mwenye umri wa miaka 34, amepitia majaribio kumi ya matibabu ya IVF katika kipindi cha miaka 10 iliyopita - lakini anasema hatimaye imelipa kwa kuweza kumpata binti yake wa miujiza.
Anna, anayefanyika kwenye taasisi ya kusaidia saratani ya Maximillan, na anayeishi mjini Hull pamoja na mumewe Phil, mwenye miaka 40, askari wa zimamoto, alisema: "Imekuwa mapambano ya ajabu ya kiroho kumpata Esme na kulikuwa na muda mwingi ambao nilifikiri kuwa siwezi kuja kuwa mama.
"Amenigharimu fedha nyingi, lakini amekuwa anathamani kwa kila senti. Ni binti yetu wa miujiza."
Mapambano ya Anna yalianza tangu mwaka 2002, pale alipoanza kujaribu kupata mtoto akiwa na mpenzi wake wa zamani.
Alisema: "Alikuwa na matatizo kadhaa ya urutubishaji na kisha nami pia ikagundulika mirija yangu ya uzazi nayo imeziba, hivyo nikajua kwamba tunahitajika kupata matibabu."
Anna alifanyiwa jaribio la kwanza la IVF kwenye zahanati ya upandikizaji mimba mjini Hull, lakini halikufanikiwa.
Kisha akafanyiwa uhimilishaji bandia, lakini tena hiyo haikufanya kazi.
Alisema: "Nilikuwa na matumaini makubwa mno mwanzoni kwamba itafanikiwa, na pale iliposhindikana, iliniteketeza.
Kisha pale jaribio la pili nalo liliposhindikana, ilinikatisha tamaa. Lakini nilidhamiria kuendelea. Nilitaka kuwa na mtoto zaidi ya chochote kile katika dunia hii."
Kisha tena akafanya majaribio mengine matano kuanzia Novemba 2005 hadi Aprili 2007. Lakini akashindwa kupata ujauzito.
Alisema: "Madaktari walishindwa kuelewa nini hakikuwa sawa. Mayai yangu mara zote yalikuwa ya ubora wa hali ya juu lakini bado hakuna kilichofanyika. Hatimaye wakanishauri nifikirie tu kuasili huku wakifikiria haiwezekani kutokea kwangu."
Kisha Anna akaenda CARE Fertility mjini Nottingham kwa msaada. Akafanyiwa tiba ya urutubishaji - ya nane kwake -lakini pia ikashindikana.
Alisema: "Walinipa moyo kwamba nisikate tamaa, lakini bado ilivunja nguvu kushindikana tena."
Nilikuwa nimeshafanyiwa matibabu ya urutubishaji mara nane hadi sasa, na sikuambulia chochote. Nilidhani siwezi kuwa mama, lakini kitu fulani ndani yangu hakikukata tamaa.
Akafanyiwa matibabu ya urutubishaji kwa mara ya tisa Julai 2008 na kushika mimba, lakini katika namna ya kukatisha tamaa mimba ile ikatoka ikiwa na wiki 11.
Alisema: "Iliniuma sana. Baada ya miaka yote hii ya kujaribu, nimepata mimba, na kuishia kupoteza mtoto wangu. Ilinikatisha tamaa."
Anna akaachana na mpenzi wake na kukutana na mumewe Phil miezi 12 baadaye. Walifunga ndoa Juni 2011 na kuamua kufanya jaribio moja la mwisho la IVF. Aligharimia majaribio yake yaliyopita kwa kuuza nyumba yake na kuchukua mikopo.
Alisema: "Hili lilikuwa ndilo jaribio langu la mwisho. Tulikuwa na fedha kiasi kwa ajili ya harusi yetu, hivyo tuliamua kutumia hizo. Nimekuwa nikijaribu kwa muda mrefu na nilipitia matibabu mengi mno. Kama hili halitafanikiwa, basi nitalazimika kukubaliana kwamba mapambano yangu yamefikia mwisho na nisingeweza kamwe kuwa mama."
Mnamo Aprili mwaka jana, Anna akafanyiwa matibabu kwa mara ya kumi hapo CARE Fertility, na wiki mbili baadaye akagundua kuwa ni mjamzito.
Alisema: "Nilipagawa, lakini nilikuwa na hofu ya kupoteza mtoto wangu tena. Wakati wote wa ujauzito hadi nilipojifungua, nilikuwa bado nahofia kwamba nitampoteza mtoto."
Esme aliwasili duniani kwenye Hospitali ya Hull and East Yorkshire mwezi Januari, mwaka huu akiwa mwenye afya njema.

No comments:
Post a Comment