Tuesday, July 9, 2013

HATIMA YA WASHITAKIWA KESI YA EPA KUJULIKANA ALHAMISI...

Majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.
Hatima ya washitakiwa wa kesi ya wizi wa Sh bilioni sita za Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kujulikana keshokutwa wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itakapoamua kama wana kesi ya kujibu au la.
Uamuzi huo utatolewa na jopo la Mahakimu, Gabriel Mirumbe, Edsoni Mkasimongwa na Pamela Mazengo baada ya kupitia ushahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.
Endapo washitakiwa hao Johnson Lukaza na ndugu yake Mwesiga Lukaza watapatikana na kesi ya kujibu watatakiwa kupanda kizimbani kujitetea na wakiwa hawana kesi ya kujibu wataachiwa huru.
Ijumaa ya wiki iliyopita upande wa mashitaka ulilazimika kufunga ushahidi baada ya Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa kuomba ufungwe kwa sababu kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara  kwa madai ya kukosa mashahidi. Jopo hilo lilikubali ombi hilo.
Novemba 4, 2008, washitakiwa hao  walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka matano, yakiwamo ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Inadaiwa Novemba 2, 2005, jijini Dar es Salaam, walighushi hati inayoonesha Kampuni ya Kernel Limited ya Tanzania  imeruhusiwa na kampuni ya Marubani Corporation ya Japan kukusanya deni la Sh 6.3 jambo ambalo si kweli.

No comments: