Wednesday, July 3, 2013

BUSH NA OBAMA WAWAKUMBUKA WAATHIRIKA WA BOMU UBALOZI WA MAREKANI DAR...

Rais Barack Obama na George W. Bush wakielekea kuweka mashada ya maua kwenye eneo ulikotokea mlipuko wa bomu kwenye Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam, jana.
Obama na Rais mstaafu George W. Bush waliweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu ya waathirika wa shambulizi la mwaka 1998 dhidi ya Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.

Wamarekani 11 waliuawa katika shambulizi hilo lililofanywa na magaidi wa kikundi cha  al Qaeda, ambalo lilikwenda sambamba na shambulizi lingine dhidi ya ubalozi wa Taifa hilo jijini Nairobi, Kenya, ambapo mamia ya watu walipoteza maisha.
Baada ya shughuli hiyo, Obama alikwenda katika mtambo wa kufua umeme wa Symbion unaomilikiwa na Marekani, baada ya tangazo lake mwishoni mwa wiki la mpango wa umeme wenye thamani ya mamilioni ya dola za Marekani. 
Mpango huo wa miaka mitano utagharimu dola bilioni 7 wenye lengo la kupatikana kwa umeme wa uhakika katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa ubia na nchi za Kiafrika na sekta binafsi.
"Tunaanza na nchi ambazo zinaonesha maendeleo katika mageuzi ya sekta ya nishati- Tanzania, Ethiopia, Kenya, Nigeria, Ghana, Uganda, Msumbiji  na Liberia," aliwambia wafanyabiashara juzi Dar es Salaam.
"Na kwa mtazamo wa kuwa na nishati ya uhakika, tutaanza kwa kuongeza megawati 10,000 za umeme mpya ambazo zitaongeza watumiaji milioni 20 wa umeme," alisema.
Katika mkutano huo, Obama alizindua mpango wa kusaidia mataifa ya Afrika Mashariki  ya  Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda, katika kufanya biashara baina yao lakini pia na Marekani.
"Tutafanya kazi na nchi ambazo zitaboresha forodha zao na kuweka mazingira mazuri ya kibiashara mipakani, zitapunguza vikwazo na matatizo ambavyo vinazuia kuingia kwa bidhaa sokoni," alisema.
 Rais Bush alikuwa Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano wa Wake wa Marais uliofadhiliwa na Taasisi ya George W. Bush.

Wakati yeye na Obama wakihudhuria hafla  katika ofisi za Ubalozi wa Marekani, wake zao walikuwa wakishiriki Mkutano wa Wake wa Marais wa Afrika. Obama na familia yake waliondoka jana  kurudi Marekani.
Wakati Obama akiondoka nchini, Dar es Salaam bado iligubikwa na shamrashamra za ujio wa kiongozi huyo, ambapo wakazi wengi wa Jiji hilo walijitokeza kwa wingi kumlaki na kufuatilia hitimisho la ziara yake nchini.
Msafara huo ulipita barabara ya Nelson Mandela akitoka Ubungo na  kuingia barabara ya Nyerere na kwa walioshindwa kufika maeneo ya barabara hizo, walikaa kwenye baa na maduka yenye luninga na kufuatilia msafara huo hadi unaondoka nchini.
Jambo la kuchekesha katika baa moja katikati ya Jiji ambako luninga ilikuwa ikionesha tukio hilo moja kwa moja wakati Obama na mkewe Michelle wakipunga mikono kuaga, baadhi ya watazamaji kwenye baa hiyo nao waliwapungia kana kwamba wanawaona.
Si hivyo, hata baada ya ndege ya Rais huyo kuondoka kwenye ardhi ya Tanzania, vijiwe vya migahawa, mafundi viatu na mikusanyiko ya watu, mjadala uliotawala ulikuwa ni wa ziara hiyo ya kihistoria na hasa ulinzi ulivyoimarishwa.

No comments: