![]() |
| Basi la Sumry likivutwa kutoka mtoni. |
Baada ya nchi kutulia kwa muda mrefu kidogo bila matukio makubwa ya ajali, matukio hayo yameanza kujitokeza baada ya basi la Kampuni ya Sumry kutumbukia mtoni na kuua watu tisa na kujeruhi 53.
Ajali hiyo ilitokea saa 6 usiku wa kuamkia jana katika Mto Iku katika kijiji cha Sitalike wilaya ya Mlele mkoani Katavi. Basi hilo lilikuwa likitoka mjini Sumbawanga mkoani Rukwa kuja hapa, likiwa na baadhi ya abiria kutoka Mbeya.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Emmanuel Nnley alisema jana kuwa basi hilo ni aina ya Nissan Diesel namba T909 AZT, lilikuwa likiendeshwa na Stephano Chimane au Ntungu.
Alisema lilipofika katika daraja lenye kona kali na mteremko, dereva alishindwa kulimudu na kulenga daraja na kusababisha magurudumu ya nyuma kupanda ukingo wa daraja na kutumbukia mtoni, lakini dereva alitoka na kutoweka.
Alifafanua kuwa juhudi za uokoaji zilifanyika usiku huo huo na majeruhi 53 kuokolewa huku maiti tisa, wanaume watatu, wanawake watano na mtoto wa kike waliopolewa majini.
Alisema hali ya majeruhi inaendelea vizuri, isipokuwa watatu walikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Rukwa kwa matibabu zaidi. Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyeshindwa kuongoza gari, ubovu wa gari na ufinyu wa daraja.
Akizungumza na mwandishi, Ofisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Safari za Nchi kavu na Majini (SUMATRA) wa mikoa ya Rukwa na Katavi, David Chiragi, alisema basi hilo lilikuwa ÔlimeibaÕ njia, kwani leseni yake iliyotolewa mwezi jana, inaliruhusu kufanya safari za Sumbawanga-Kirando na si Sumbawanga-Mpanda.
Alisema hata upana wa daraja ilipotokea ajali hiyo ni mdogo sana, ambapo vipimo vinaonesha daraja hilo lina upana wa meta tatu na nusu, wakati basi lina upana wa meta nne na nusu, hivyo kujenga mazingira ya ugumu wa dereva kulenga daraja katika msukosuko wowote hasa usiku. Alitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Katavi, kupanua na kuboresha eneo hilo.
Aliongeza kuwa kati ya Januari na mwezi huu, zaidi ya ajali tisa zimetokea katika daraja hilo, zikihusisha magari makubwa saba na madogo mawili, kutokana na madereva kushindwa kumudu magari yao na kulenga daraja hilo.
Kamanda alisema pia basi hilo lina makosa ya kutofuata ratiba, kuiba njia na kuzidisha abiria, hivyo ofisi yake imechukua hatua ya kuzuia safari za mabasi ya Sumry mchana na badala yake yataondoka Sumbawanga na Mpanda asubuhi tu.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wakizungumza kwa tabu hospitali ya wilaya ya Mpanda jana, walidai dereva alikuwa akiendesha kwa mwendo wa taratibu sana tangu mwanzo wa safari, hali iliyowapa shaka kuwa huenda alikuwa hajui kuendesha magari.
Lakini, wapo pia waliodhani kuwa basi hilo lilikuwa na hitilafu, kwani waliondoka Sumbawanga saa 11 jioni na kufika eneo hilo saa 7.30 usiku, tofauti na mwendo wa kawaida, ambapo walitakiwa kufika hapo saa nne usiku.
Kondakta ambaye hakutaka kutaja jina lake, alidai kuwa dereva huyo ni mgeni wa njia, pia hajazoea kuendesha mabasi aina ya Nissan Diesel, hali iliyomlazimu kumwelekeza njia wakati wote wa safari.
Alidai walipofika eneo la mteremko wa Mto Iku, alimweleza kuwa mbele kuna daraja jembamba na kona kali, dereva huyo alibadili gia ikagoma na kuanza kuporomoka hadi mtoni.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk Rajabu Rutengwe alitoa rambirambi kwa wafiwa na kuwapa pole majeruhi.

No comments:
Post a Comment