Wednesday, July 24, 2013

ASKARI KUTOKA ZANZIBAR WALIOUAWA DARFUR WAZIKWA...

Askari wakiwa wamebeba moja ya majeneza yenye miili ya wanajeshi hao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein jana   aliungana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa vikosi vya ulinzi na usalama wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wafiwa na wananchi katika maziko ya wanajeshi wa Zanzibar waliouawa Darfur, Sudan.
Wanajeshi hao,  Sajenti Shaib Shehe Othman na Koplo Mohammed Juma Ali miili yao ilizikwa eneo la Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja   katika makaburi yaliyochimbwa  sambamba. Marehemu wote walizikwa kwa taratibu za kijeshi na baadaye kufuatiwa na taratibu za kidini.
Awali, Dk Shein pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad walishiriki katika dua ya hitma iliyosomwa kwa ajili ya miili ya wanajeshi hao katika Msikiti wa Noor Mohammad uliopo eneo la Mombasa kwa Mchina, Mkoa wa Mjini Magharibi,  Unguja.
Rais alisaini vitabu vya maombolezo kwa ajili ya marehemu hao katika eneo hilo la Msikiti kabla ya kushiriki maziko kwenye makaburi licha ya viongozi, ndugu, jamaa na marafiki, pia wanajeshi wa kikosi cha Ulinzi cha JWTZ walijipanga makaburini hapo kwa ajili ya kuaga wenzao kwa mila, desturi na taratibu zote za kijeshi.
Viongozi wengine walioshiriki maziko ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,  Shamsi Vuai Nahodha, wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama vya SMT na SMZ na wananchi pamoja na wafiwa.
Baada ya maziko, salamu za Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya  Kikwete zilitolewa kwa  wafiwa na wanafamilia wa marehemu  ikielezwa msiba huo ni wa taifa zima na si kwa upande wa Tanzania pekee bali  Afrika na dunia nzima.
Wanafamilia na wazazi wa marehemu hao, walitoa shukurani zao za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi kubwa ilizozichukua kuhakikisha marehemu hao wanafika katika maeneo yao ya kuzikwa kwa kufanikisha taratibu zote za usafiri kwa ufanisi mkubwa.
Walishukuru pia hatua ya Serikali kuwezesha kupata taarifa kwa kila hatua iliyokuwa ikichukuliwa katika mchakato wote wa usafiri wa watoto wao hao tangu wakiwa Sudan hadi walipowasili nchini na kuzikwa visiwani hapa.

No comments: