![]() |
| Dk William Mgimwa. |
Bunge jana lilipitisha Bajeti ya Serikali ya Sh
trilioni 18.2 kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa na wabunge wa Bunge hilo na kuiwezesha
Serikali sasa kuanza kazi rasmi Julai mosi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na meza ya
Katibu wa Bunge, wabunge waliopiga kura hiyo kwa kuhojiwa mmoja baada ya
mwingine, ni 270 kati ya wabunge 354 ambao ndiyo idadi ya jumla ya wabunge hao.
Wabunge waliosema hapana ni wabunge 35 na waliokubali
ni wabunge 235 huku wabunge 83 wakiwa hawamo katika ukumbi wa Bunge wakati kura
hiyo ikipigwa baada ya wabunge kuitwa kuingia ndani kwa kengele.
Baada ya kura hiyo na matokeo kutangazwa, Spika Anne
Makinda alisema sasa Serikali itaanza kazi yake Julai mosi, huku akihimiza
fedha zilizopitishwa zifanye kazi iliyokusudiwa ili kuwaletea maendeleo
wananchi.
Alisifu Serikali kwa kufanya kazi kubwa kwa kukubali
kubadilisha baadhi ya mambo ambayo yalishafikishwa katikati.
Alisema wakati bajeti inajadiliwa ni vema kuzingatia
maslahi ya wapiga kura bila kuangalia tofauti za kivyama ndani ya Bunge hilo.
Mapema akifanya majumuisho, Waziri wa Fedha, Dk
William Mgimwa, alipongeza wabunge waliochangia na kuahidi kuwa hoja zao
zimefanyiwa kazi na Serikali na hivi punde wakati wa kujadili sheria ya fedha
zitatolewa majibu.
Baadhi ya hoja hizo ni za kupunguza kodi katika baadhi
ya maeneo na pia kuangalia upya mapendekezo ya kupunguza kodi kwenye pikipiki
za biashara-bodaboda, simu za mkononi ambazo pia zimekuwa zikitumiwa kutuma
fedha. Hata hivyo alisema Bajeti yake inajielekeza zaidi vijijini.
Akijenga hoja kwa nini ni bajeti ya vijijini, Mgimwa
alisema anataka wananchi vijijini wanufaike kwa kutoa kipaumbele katika
mahitaji ya wananchi hao.
Mahitaji ya umeme vijijini yameongezwa fedha zaidi kwa
mujibu wa Mgimwa, ambapo sasa Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA), iliyokuwa
imepangiwa Sh bilioni 153 katika bajeti ya awali, imeongezwa Sh bilioni 186,
ili ipeleke umeme vijijini.
Katika sekta ya maji, alisema Serikali imekubali
kuongeza Sh bilioni 184, sekta ya miundombinu ya usafirishaji ikiongezwa
Sh bilioni 30 huku Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (EPZ), yakiongezwa Sh bilioni
30, ili kukuza uwekezaji na sekta ya mifugo ikiongezwa Sh bilioni 20.
Tofauti na ilivyotarajiwa na wengi, kwamba Waziri
Mgimwa, angefafanua kama amepunguza kodi au la katika maeneo
yaliyotarajiwa zaidi kama mafuta jamii ya
petroli, Waziri aliwataka wabunge wasubiri ufafanuzi.
Hoja zilizotakiwa kusubiri ufafanuzi wakati Muswada wa
Sheria ya Fedha utakapoletwa keshokutwa, bila kufafanua kama zimekubaliwa kama wabunge walivyoomba au la, ni pamoja na ombi
la punguzo la kodi ya mshahara la asilimia moja, kuongezwa hadi asilimia 3.
Nyingine ni kodi katika petroli na dizeli, ambayo
ilipendekezwa na Kamati ya Bajeti na baadhi ya wabunge kwamba kusiwepo nyongeza
ya aina yoyote ya kodi katika bidhaa hizo.
Katika Bajeti ya Serikali, ilipendekezwa kuwa ushuru
katika mafuta ya dizeli uongezwe kwa Sh 2 kwa kila lita kutoka Sh 215
inayotozwa sasa mpaka Sh 217.
Katika petroli, Serikali ilikusudia kuongeza ushuru wa
Sh 61 kwa kila lita, kutoka Sh 339 inayotozwa sasa kwa kila lita, mpaka Sh 400
kwa lita.
Mgimwa katika majibu yake ya jana, hakusema kama
amekubaliana na wazo hilo
la Kamati ya Bajeti na baadhi ya wabunge, badala yake alisema amelishughulikia
na atafafanua zaidi wakati wa Muswada wa Sheria ya Fedha.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kazi iliyofanyika katika
mafuta ya petroli, imezingatia kuzuia uchakachuaji, jambo linaloonesha, ushuru
wa mafuta ya taa yaliyokuwa yakitumika kuchakachua dizeli, hautashuka.
Kuhusu kodi ya mshahara, Mgimwa alitoa historia ya
kupunguza kodi hiyo kuanzia mwaka 2007/08 ilipokuwa asilimia 18.5 katika kima
cha chini mpaka asilimia 14 mwaka huu wa fedha na sasa kusudio ni
kupunguza kwa asilimia moja mpaka 13.
Kamati ya Bajeti, ilitaka ipungue kwa asilimia tatu
mpaka 10 lakini Mgimwa alisema Serikali itaendelea kutafuta namna ya kupunguza
kodi hiyo.
Kuhusu mapendekezo ya Serikali kuongeza ushuru katika
huduma zote za simu kutoka asilimia 12 ya sasa hadi 14.5 kwa mwaka ujao wa
fedha, Kamati ya Bunge ilishauri nyongeza ya asilimia 2.5 ifutwe, lakini Mgimwa
alisema, atafafanua katika Sheria ya Fedha.
Katika ushuru wa bodaboda wa barabara, ambao Serikali
ilitaka kuusamehe na wabunge kupinga kwa maelezo kwamba
watakaofaidika si vijana wanaoziendesha wanaolengwa, bali wamiliki wa usafiri
huo, Mgimwa alisema amelifanyia kazi na itaonekana katika Sheria ya Fedha,
baada ya kuupata ukweli kutoka kwa vijana hao.
Wakati huo huo Chadema, ilitoa taarifa jana kuwa
imegoma kuhudhuria kikao cha kupitisha Bajeti kwa madai kwamba, Bunge
haliwajali, halikusitisha shughuli zake kuomboleza, wala halikutoa hata pole.
Pia walidai walinyimwa kusoma maoni yao,
kwa kuwa awali bajeti ilitakiwa kupitishwa leo, badala ya jana.
Wakati wabunge wa Chadema walipokuwa
wakiitwa kukubali au kukataa bajeti, wabunge wa CCM walifungua vipaza sauti na
kusema “maandamano”.

No comments:
Post a Comment