![]() |
| George Mkuchika. |
Serikali imefanikiwa kuokoa jumla ya Sh.bilioni 3.2
kutokana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kusimamisha malipo baada ya kuonekana kuwa si halali.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Utawala Bora), George Mkuchika juzi alipokuwa akitoa neno la shukrani kwenye
sherehe ya kuwaaga viongozi na watumishi wa Tamisemi, waliohama na kustaafu.
Mawaziri waliohama Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi ni
Celina Kombani ambaye sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais Utumishi na George
Mkuchika ambaye alitoka Ofisi ya waziri Mkuu Tamisemi kwenda Waziri wa Nchi
Ofisi ya rais Ikulu.
Wengine walioagwa na kupongezwa ni makatibu wakuu
waliohama ofisi wa waziri mkuu, Makatibu tawala wa Mikoa na
wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa waliostaafu, watumishi
waliostaafu ofisi ya Waziri Mkuu na watumishi waliohama
Jumla ya watumishi waliotakiwa kutunukiwa zawadi
walikuwa 59 lakini waliohudhuria sherehe hizo walikuwa 35 ambapo zawadi
mbalimbali zilitolewa ikiwemo, seti za televisheni, picha kubwa za ukutani za
nyumba za asili, na zawadi nyingine.
Akizungumza Waziri Mkuchika alisema ipo kero ya rushwa
na wizi katika halmashauri mbalimbali nchini na wakati mwingine wafanyakazi wa
wizara wanashirikiana na watendaji wa halmashauri kufanya vitendo hivyo
viovu.
Mkuchika alisema kwamba fedha hizo zilizookolewa
zilikuwa zinapotea kutokana na kuwapo kwa rushwa katika shughuli zilizofanywa
na halmashauri mbalimbali.
Kutokana na tatizo hilo Mkuchika amewataka Watendaji
wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
kujiepusha na rushwa kwani kumekuwa na vitendo vya wafanyakazi wa wizara
kushirikiana na watendaji wa halmashauri katika wizi huo.
Alisema sasa kazi aliyopewa ni kuangalia halmashauri
zinavyokwenda na kuwataka watendaji kushikilia rekodi ya hati safi kwenye halmashauri na kujiepusha na
vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikifanywa na watu wa Wizarani na
halmashauri.
“Wizara niliyohamia inajishughulisha na kupambana na
rushwa isije ikawa umepita huko mambo yakawa mabaya ukaja Mzee naomba
nisaidie kwa hilo
sitakuwa na msaada kila mtu analinda kitumbua chake” alisema.
Mkuchika alisema tangu mkaguzi mkuu alipoanza kukagua
vitabu vya halmashauri nusu ya hati zilikuwa chafu lakini katika ukaguzi wa
mwaka jana kuna hati moja tu ambayo ilitokana na kula njama kati ya mtumishi wa
halmashauri na mtumishi wa Wizarani.
“Mara chache mtu kusimama na kuipongeza Tamisemi, kuna
halmashauri zaidi ya 130 nchini na kupatikana hati chafu moja tu ni mafanikio
makubwa katika utendaji” alisema
Alisema ni lazima ukifanya kazi Tamisemi ukubali lawama
kwani ni wizara inayojishughulisha na watu na maisha ya watu hivyo uadilifu ni
jambo linalotakiwa ili kuweza kuondoa malalamiko katika wizara hiyo.
Mkuchika ambaye alipewa zawadi ya televisheni ya
inchi 32 na picha ya ukutani, alimpongeza Waziri Mkuu kwa zawadi hiyo kwani
televisheni yake aliyokuwa ameiweka chumbani kwake iliungua mwezi mmoja
uliopita.
“Nashukuru sana kwa
zawadi hii lazima niseme ukwei TV niliyokuwa nimeweka chumbani ambayo ilikuwa
ikinipa fursa ya kuangalia mapitio ya magazeti kila asubuhi ilikuwa imeungua kama mlijua hitaji langu” alisema
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa
Mstaafu, Getrude Mpaka alisema alitaka serikali kuweka msisitizo wa kozi za
wastaafu ili waweze kujiandaa na pia serikali iwaandae wastaafu kuwa na gari na
nyumba.
Akizungumza katika sherehe hizo, Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, alisema hiyo ni fursa nzuri ya kubadilishana mawazo kwa wale waliostaafu
na kutakiana kila la kheri kwa wale ambao wamehamishiwa kwenye taasisi
nyingine.
Alisema kufanya kazi kipindi chote hadi kustaafu
salama ni jambo jema kutokana na utumishi wa umma kuwa na changamoto nyingi .
“Waulizeni wastaafu mara ngapi wamesingiziwa mambo ya
ovyo huyo Chadema au huyo CUF na anayesema hivyo utadhani ni msafi sana.” Alisema
Alisema wale waliohamishiwa maeneo mengine
serikali imeona utendaji wenu kuwa mnaweza kuleta mabadiliko kwenye taasisi na
maeneo mapya mliyopangiwa.
Waziri Mkuu alisema Chama cha Wafanyakazi
(TUCTA), wameanzisha wazo ambalo ni zuri la kuandaa watumishi kustaafu na
mtumishi anapofanya kazi kwa audilifu lazima apongezwe.

No comments:
Post a Comment