![]() |
Msanii Langa Kileo. |
Msanii maarufu wa Hip Hop, Langa Kileo maarufu kama Langa, amefariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa baadhi ya ndugu wa marehemu ambao hawakutaka kutajwa majina yao, walithibitisha na kuongeza kwamba Langa amefariki kutokana na ugonjwa wa malaria aliokuwa akitibiwa kwenye hospitali hiyo.
Langa ambaye katika miaka ya hivi karibuni alikuwa akituhumiwa kwa matumizi ya dawa za kulevya, aliwahi kukiri hadharani alipohojiwa na vituo kadhaa vya redio hapa nchini na kuanika mipango yake ya kuendesha vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo kwa vijana.
Mbali na hilo, Langa alitangaza kufungua kituo maalumu cha kutoa elimu kwa vijana dhidi ya utumiaji wa dawa za kulevya. Pia alijitangaza kuwa balozi wa kupambana na dawa za kulevya.
Msanii huyo alichomoza kwenye anga la muziki kufuatia mashindano ya Coca-Cola Pop Star yaliyofanyika Afrika Kusini mwaka 2004 na kushirikisha nchi tatu za Afrika Mashariki.
Kundi lao la Wakilisha lililojumuisha wasanii watatu, yeye Langa, Sarah Kaisi 'Shaa" na Witness Mwaijaga lilishika chati za muziki na kujizolea umaarufu kupitia nyimbo zake za 'Kiswanglish' na 'Waniacha Hoi'.
No comments:
Post a Comment