Thursday, June 13, 2013

HII NDIO BAJETI YA ZANZIBAR, UCHUMI WAPANDA KWA ASILIMIA 7.5...

Omar Yussuf Mzee.
Serikali ya Mapinduzi ya imetangaza bajeti ya fedha kwa mwaka 2013-2014 huku ikiweka kipaumbele  dira ya maendeleo ya 2020 pamoja na mpango wa kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini, MKUZA, kama ndiyo kipaumbele cha kuleta maendeleo.
Akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013-2014 Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughukilia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee alisema hali ya uchumi ya Zanzibar imezidi kuimarika na kufikia asilimia 7.5 kutoka 6.7 katika mwaka 2012.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2012-2013 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kutekeleza miradi minne katika sekta ya maji safi na salama, afya, ajira na elimu.
Mzee alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo Serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 113.2, huku akiitaja sekta ya Afya imetengewa Sh bilioni 23.9,sekta ya Maji safi na salama imetengewa Sh bilioni 55.4 pamoja na ajira kwa vijana zimetengwa jumla ya Sh bilioni 1.1.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2013-2014 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajiwa kutumia jumla ya Sh bilioni 658.5 ikilinganishwa na bajeti iliyopita ya mwaka 2012-2013 ya jumla ya Sh bilioni 648.9.
Akifafanua alisema bajeti hiyo asilimia 50 inategemea makusanyo ya vyanzo vya mapato vya ndani vinavyokusanywa na taasisi za kukusanya mapato nchini Bodi ya mapato na Mamlaka ya kodi nchini TRA.
Alisema katika mwaka 2013-2014 ukusanyaji wa mapato ya Serikali unatazamiwa kufikia asilimia 21.3 yaani Sh bilioni 324.6 huku ZRB ikiwekewa malengo kukusanya Sh bilioni 171.7 na TRA kukusanya jumla ya Sh bilioni 147.9.
Mzee alisema Serikali inatazamiwa kukusanya mapato katika vyanzo vyake vya ndani jumla Sh bilioni 333.7.
Alisema katika mikakati ya kuhakikisha Serikali inakusanya mapato yake vizuri, Serikali itadhibiti misamaha ya kodi ambayo ilikuwa ikilikosesha taifa zaidi ya Sh bilioni 12.6.
Mzee alisema unafuu wa misamaha kwa asilimia 100 utatolewa kwa ofisi za kibalozi na miradi inayotokana na wafadhili wa washiriki wa miradi ya maendeleo.
Alisema taasisi nyengine unafuu utatolewa kwa asilimia 80 na asilimia 20 iliyobaki ndiyo itakayolipiwa kodi , ambapo alisema hatua hiyo itaongeza mapato kwa Sh bilioni 4.56.
Mapema Mzee alisema serikali inakusudia kuzifanyia marekebisho viwango vya kodi kwa ajili ya kuongeza mapato na kuacha utegemezi kutoka kwa wafadhili na washiriki wa maendeleo.
Alizitaja kodi zitakazofanyiwa marekebisho na kupanda ikiwemo ada ya bandari kwa wasafiri wa baharini na uwanja wa ndege pamoja na ushuru wa stempu na kodi za leseni ya udereva.
Alisema ada ya viwanja vya ndege itapanda ili kufikia viwango vya nchi za Afrika ya mashariki dola za kimarekani 35 na kufikia 40 kwa mtu na hivyo kusaidia mapato na kufikia Sh bilioni 1.2.
Aidha kodi za mahoteli zinatazamiwa kufanyiwa marekebisho ili kudhibiti ukwepaji wa  kodi unaofanywa na wamiliki wa mahoteli wasiokuwa waaminifu wakati wanapofanyiwa ukaguzi.
Aidha Mzee Serikali inakusudia kudhibiti na kupambana na magendo ya mafuta nchini ambapo mashirikiano yamefikiwa kati ya TRA pamoja na ZRB na Mamlaka ya Mapato ya Kenya.
Mapema Mzee aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao katika mchakato wa marekebisho ya katiba kwa njia ya amani na kuepuka fujo.
Alisisitiza na kusema kwamba Muungano wa Tanganyika ulioasisiwa na viongozi wawili Abeid Amani Karume na Mwalimu Nyerere ndiyo kielelezo cha taifa la Tanzania.
'Nawaomba wananchi wa Zanzibar kutoa maoni katika mchakato wa katiba ya Tanzania kwa njia ya amani na utulivu....Muungano wetu ndiyo kielelezo cha taifa hili huku umuhimu wake ukionekana kwa kila pande,"alisema.
Akizungumzia kuhusu  maslahi ya wafanyakazi, Mzee alisema ahadi ya rais wa Zanzibar katika kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wote bado ipo pale pale.
Alisema katika bajeti  ya mwaka wa fedha 2013-2014 Serikali imetenga jumla ya Sh bilioni   17.5 kwa ajili ya maslahi ya wafanyakazi ikiwemo nyongeza ya mishahara.
'Katika bajeti hii tumetekeleza ahadi ya rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein katika kuimarisha maslahi ya wafanyakazi wote nchini,'alisema.
Aidha Mzee aliitaja bajeti ya mwaka wa fedha 2013-2014 kuwa ni bajeti nafuu kwa wananchi baada ya serikali kufanikiwa kukamilisha miradi mbali mbali, ikiwemo wa nishati ya umeme kutoka Ras Kilomoni Tanzania Bara hadi Fumba na ule wa Pemba hadi Tanga.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kumeleta unafuu mkubwa kwa wananchi ikiwemo kutumia nishati ya umeme kwa maendeleo ya taifa.

No comments: