Monday, May 13, 2013

WILSON MASILINGI ATEULIWA BALOZI MPYA UHOLANZI...

Wilson Masilingi.
Hatimaye Rais Jakaya Kikwete ametimiza ahadi yake ya kufungua ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi, kwa kumteua mbunge na waziri wa zamani, Wilson Masilingi kuiwakilisha nchi katika Taifa hilo la Ulaya.

Hivi karibuni Rais Kikwete alikuwa ziarani nchini humo ambako pamoja na mambo mengine, aliahidi kufungua ubalozi huo.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, ilisema Rais alifanya uteuzi wa mabalozi wapya na kujaza nafasi zilizokuwa wazi na kuanzisha ofisi hiyo ya Uholanzi na ya Comoro na kufanya uhamisho wa Balozi mmoja.
Pamoja na Masilingi ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Chabaka Kilumanga naye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro akitoka kuwa Balozi Mdogo wa Tanzania nchini Uingereza.
Masilingi alipata kuwa Mbunge kati ya mwaka 1995 hadi  2010  ambapo pia katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2005 alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora.
Katika uteuzi huo, taarifa pia ilisema Modest Mero aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa, Geneva, akitoka kuwa Ofisa wa Mambo ya Nje Mwandamizi kwenye Ubalozi wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa, New York.
Rais pia amemhamisha Balozi Philip Marmo kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China na kwenda Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.

No comments: