![]() |
Wilfred Rwakatare. |
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Rwakatare leo anapandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kufutiwa mashitaka ya ugaidi, yaliyokuwa yanamkabili.
Mei 8 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilimfutia Rwakatare na mshitakiwa mwenzake, Ludovick Joseph mashitaka matatu ya ugaidi, yaliyokuwa yakiwakabili.
Hatua hiyo inatokana na ombi la Rwakatare, la kutaka Mahakama hiyo ifanye marejeo ya mwenendo wa kesi ya ugaidi, baada ya Mkurugenzi kuwafutia mashitaka kisha kuwakamata na kuwashitaki kwa mashitaka yaleyale.
Kutokana na uamuzi uliotolewa na Jaji Lawrence Kaduri, Rwakatare na Joseph wanakabiliwa na mashitaka ya jinai, chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambayo yanaruhusu dhamana.
Katika mashitaka hayo, washitakiwa hao wanadaiwa Desemba 28 mwaka jana katika eneo la King’ongo, Kinondoni, Dar es Salaam walipanga njama ya kutenda kosa la jinai la kutumia sumu kumdhuru Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika. Mahakama hiyo ilikuwa inasubiri jalada la kesi, ambalo lilikuwa kwa DPP ili iwasomee washitakiwa maelezo ya kesi kabla ya kuihamishia katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Washitakiwa hao, walifutiwa mashitaka ya kupanga njama za kufanya kitendo cha ugaidi cha kumteka Msacky, kupanga na kushiriki mkutano wenye lengo la kutenda kitendo cha ugaidi, ambacho ni kumteka Msacky.
Aidha, Rwakatare alifutiwa mashitaka ya kuruhusu mkutano kati yake na Joseph, kufanyika nyumbani kwake katika eneo la King’ongo, Kimara Stop Over, kwa lengo la kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Jaji Kaduri alifuta mashitaka hayo, kwa kuwa hati ya mashitaka iliyofunguliwa na DPP, haielezi uhalisia wa kosa hilo na washitakiwa wanahusika vipi kufanya ugaidi. Na kufafanua kuwa, “Hati ya mashitaka lazima itoe uhalisia wa kosa husika (ugaidi) ili haki itendeke”.
Aidha, alisema washitakiwa hawakufanya mkutano wa kigaidi, kama inavyodaiwa, kwa kuwa walikuwa wawili na kisheria mkutano wa kigaidi, unahusisha watu zaidi ya watatu.
No comments:
Post a Comment