![]() |
Mawaziri (kutoka kushoto) Dk John Magufuli, Dk Abdallah Kigoda na Dk Harisson Mwakyembe. |
Mawaziri watatu wenye taaluma za udaktari, John Magufuli, Abdallah Kigoda na Harrison Mwakyembe, wiki hii wanatarajiwa kuwa ‘kikaangoni’ wakati Bunge litakapojadili makadirio ya matumizi ya wizara zao kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Watatu hao wamepewa na Rais Jakaya Kikwete jukumu la kusimamia Wizara za Ujenzi, Viwanda na Biashara na Uchukuzi.
Wa kwanza atakuwa Dk Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi, na leo atakuwa kilingeni akitetea wizara hiyo, ambapo kwa siku mbili Bunge litajadili makadirio yake.
Atafuatiwa na Dk Kigoda wa Viwanda na Biashara ambaye kwa siku moja ya Jumatano, makadirio yake yatajadiliwa na Bunge na endapo yataridhisha, basi watayapitisha.
Atakayefunga mjadala kwa wiki hii ni Dk Mwakyembe, ambaye kwa mara ya kwanza atasimamia bungeni kuwasilisha Makadirio ya Matumizi na atafanya hivyo akiwa na dhamana ya uchukuzi.
Kwa Dk Magufuli, masuala ambayo yanatarajiwa kurindima kwake ni jinsi Serikali ilivyojipanga kutekeleza miradi ya barabara kwa mwaka ujao wa fedha, eneo ambalo imekuwa ikifanya vizuri.
Hadi sasa, barabara nyingi hasa zinazounganisha mikoa, zimekamilika isipokuwa chache kama za Tabora na Kigoma, Mara na Arusha, na ambazo Dk Magufuli anatarajiwa kueleza mipango ya utekelezaji inavyoendelea.
Hata hivyo, masuala ya makandarasi na wajenzi pia yatachukua nafasi katika wizara hii hasa baada ya hivi karibuni, Tanzania kushuhudia kuanguka kwa jengo la ghorofa 16 Dar es Salaam.
Kwa Viwanda na Biashara, kwa Dk Kigoda, pia mjadala utakuwa mkubwa kutokana na ukweli kuwa hiyo ni moja ya sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa, hivyo mjadala wake unatarajiwa kuwa mkali keshokutwa.
Dk Mwakyembe ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi chini ya Dk Magufuli ana mengi ya kulieleza Bunge na pia mengi yanasubiriwa kutoka kwa wabunge, kwani anaongoza sekta nyingine nyeti nchini, Uchukuzi.
Masuala ya usafirishaji kwa maana ya reli, bandari, usafiri wa anga na ya hali ya hewa, ni miongoni mwa majukumu ya wizara hii, hivyo unyeti wake huo na umuhimu kwa ustawi wa Taifa, utafanya kuwapo kwa mjadala mkali kwa siku mbili ilizopangiwa Wizara ya Uchukuzi kuanzia Alhamisi.
Mkutano huu wa 11 wa Bunge, utaendelea wiki hii baada ya wiki iliyopita kushuhudia mjadala mkali katika wizara tatu nyingine kutokana na kugusa hisia za wabunge wengi waliochangia mijadala hiyo.
Hizo ni za Mambo ya Ndani ya Nchi, iliyoshuhudia mjadala mkali kuhusu uvunjifu wa amani nchini hasa kuibuka kwa chokochoko za kidini, bajeti ndogo kwa Jeshi la Polisi na suala la amani ya nchi kwa ujumla wake.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nayo ilikuwa na mjadala mkali kutokana na umuhimu wa afya kwa kila binadamu na wabunge kumalizia wiki kwa kujadili masuala ya akinamama, watoto na jinsia kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto chini ya Waziri Sophia Simba.
No comments:
Post a Comment