WABUNGE WANNE WA CHADEMA WASHINDIKANA BUNGENI...

Kikao cha Bunge kikiendelea mjini Dodoma.
Wabunge wanne wa Chadema wamebainika kuhusika na utovu wa nidhamu bungeni, uliojitokeza wiki iliyopita na kusababisha vurugu.
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyopewa kazi ya kuchunguza mazingira yaliyochangia uvunjifu wa kanuni pamoja na wabunge waliohusika, ilitoa taarifa yake jana bungeni na kuwataja wabunge hao. 
Wabunge hao  hata hivyo, wamewekwa kiporo kusubiri Kamati ikutane nao kabla ya kuamua ni adhabu gani wapewe. Wabunge hao ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Pauline Gekul (Viti Maalumu)  na John Mnyika (Ubungo).
Akiwasilisha taarifa ya kamati, Mwenyekiti Hassan Ngwilizi alisema kwa kutumia ushahidi wa picha za video zilizopigwa na TBC na kumbukumbu za Bunge, ilibaini wabunge waliokuwa wakisimama,  kuwasha vipaza sauti na kujibizana na kiti cha Spika kinyume na kanuni.
Ngwilizi alisema Mnyika alisimama mara kadhaa akiomba utaratibu licha ya Kiti kutomruhusu, hali iliyodhihirisha utovu wa nidhamu.
Kwa upande wa Lissu, Nassari na Gekul, walibainika kuzungumza kwa jazba kwamba ‘mnatuburuza’ na kuamsha ari kwa wabunge wengine hali iliyoibua vurugu.
Ngwilizi alisema Nassari alikishambulia na kujibizana na Kiti cha Spika akimwambia anabaka kanuni.
Wakati miongoni mwa adidu za rejea ni mazingira yaliyochangia vurugu, Kamati ilibaini kwamba tafsiri ya muda aliotumia Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe ndicho kilikuwa chanzo cha vurugu.
Hata hivyo Kamati ilisema muda aliotumia Waziri Maghembe wa dakika 30 ulikuwa sahihi kulingana na kanuni, tofauti na Lissu alivyohoji akidai anapaswa atumie dakika 15. “Hatua ya kuhoji Kiti kuhusu muda haikuwa sahihi bali kukilazimisha,” alisema.
Kamati ilisisitiza kwamba Naibu Spika, Job Ndugai alikuwa sahihi kuondoa hoja bila mjadala. Alisema hoja ilifika hatua ya kujadiliwa na ilikuwapo dhamira isipokuwa mtoa hoja (Mnyika) alifanya fujo.  “Kilichokosekana ni hali ya utulivu na si kukiukwa kanuni,” alisema.
Ingawa Kamati ya Ngwilizi yenye wajumbe 16 ilipewa kazi ya kutoa maoni na mapendekezo, katika taarifa yake haikufanya hivyo. Hata hivyo Spika Anne Makinda alisema Kamati haikufanikiwa kukutana na wabunge waliobainika kuhusika na utovu wa nidhamu.
Alisema katika kuzingatia utawala bora, Kamati itakutana na kila mmoja kabla ya kuamua hatua za kuchukuliwa dhidi yao. “Kama Kamati ingekutana nao, tungechukua hatua,” alisema Makinda.
Kanuni ya  74 inataja adhabu zinazoweza kutolewa na Spika kwa ukiukaji wa kanuni inaweza kushauri ikiwa ni kosa la kwanza, mbunge asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi 10.
Ikiwa ni la pili au zaidi mbunge huyo hatahudhuria vikao vya Bunge visivyozidi 20. Hata hivyo, bila kujali ushauri wa Kamati, Bunge linaweza kumchukulia hatua nyingine za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi mbunge  aliyetenda kosa.

No comments: