SPIKA MAKINDA AMWAGIWA MATUSI YA NGUONI KWENYE SIMU...

Spika Anne Makinda.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amepokea matusi ya nguoni kutoka kwa watu walioshawishiwa na Chadema, kumshinikiza ajiuzulu.
Matusi hayo yalianza kumiminika kuanzia juzi, baada ya viongozi wa Chadema kutangaza namba za simu za Spika kwenye mkutano wa hadhara na kuendelea jana, ili kutumia inayoitwa ‘nguvu ya umma’, kumlazimisha ajiuzulu.
Hadi jana mchana, mtoa habari wetu ambaye yuko karibu na Spika Makinda, alisema simu za kiongozi huyo wa Bunge, zilikuwa zimepokea zaidi ya ujumbe mfupi wa maneno 400, kutoka kwa watu wasiojulikana.
Ujumbe huo kwa mujibu wa mtoa habari wetu, ulitawaliwa na matusi ya nguoni ya kila namna dhidi ya Makinda binafsi na simu zaidi ya 200 kutoka kwa watu wasiojulikana zilirekodiwa.
Kisa cha matusi hayo, ni hatua ya Spika Makinda kutangaza mabadiliko ya Kamati za Bunge, yaliyoivunja Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na shughuli zake kuwekwa chini ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kutokana na mabadiliko hayo, aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), hakuridhishwa na kuamua kutafuta alichokiita namna ya kumng’oa Spika Makinda.
Moja ya mbinu aliyotumia Zitto ni taarifa kwa vyombo vya habari juzi asubuhi, ikihimiza ang’olewe madarakani kwa kutangaza uamuzi huo wa Bunge.
“Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge,” alieleza Zitto katika taarifa hiyo.
Baada ya taarifa hiyo, Zitto alishiriki maandamano ya viongozi na mashabiki wa Chadema Dar es Salaam na katika mkutano wa hadhara uliofanyika Temeke.
Katika mkutano huo, alizungumzia mbinu na mikakati ya kumng’oa Spika Makinda kwa sababu hiyo hiyo ya kutangaza mabadiliko ya muundo wa kamati za Bunge, yaliyomwathiri Zitto binafsi.
“Kuna njia za kumng’oa Spika Makinda, kwanza kwa kupeleka hoja ya kutokuwa na imani naye na nimeambiwa hapa kwamba imeshakamilika. Au tuandamane hadi pale shule ya msingi Bunge…au tutumie namba zake kumpigia na kumtumia ujumbe wa simu za mkononi,” alikaririwa Zitto na vyombo vya habari katika mkutano huo.
Baada ya kutamka mbinu hizo, Zitto alimruhusu Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kutaja namba za Spika Makinda na Naibu wake, Job Ndugai.
Wakati Zitto akishawishi wananchi kumng’oa Spika Makinda kwa kutumia ujumbe wa simu, ambapo sasa imegeuka na kuwa matusi, alisema uamuzi wa kuvunja kamati ya POAC ni wa Spika Makinda, jambo ambalo si kweli.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah, alipozungumza na gazeti hili juzi, alisema uamuzi huo haukufanywa na Spika Makinda peke yake, bali ni baada ya kushauriana na Kamati ya Kanuni za Bunge, ambayo iliridhika na sababu za kuchukuliwa uamuzi huo.
Wajumbe wa Kamati iliyoridhia makubaliano hayo mbali na Spika na Naibu Spika, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Wengine ni Mbunge wa Mbulu, Mustapha Akunaay (Chadema), Mbunge wa Kibondo, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF).
Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM), Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM).
Dk Kashilillah alisema mabadiliko hayo hayakuigusa kamati ya POAC peke yake, bali kamati zingine kama ya Sheria Ndogo na ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, ambayo imegawanywa mara mbili.
Akielezea sababu za kuvunja POAC, Dk Kashilillah alisema lengo lilikuwa ni kuunganisha wizara, taasisi zake na mashirika yaliyo chini ya wizara husika, ili yawe na msemaji mmoja.
Alisema awali Waziri alikuwa anawajibika PAC, wakati mashirika ya umma yaliyo chini ya wizara yakiwajibika chini ya POAC.
Kwa mujibu wa Dk Kashilillah, kulikuwa na mkanganyiko mkubwa na akaeleza kuwa hatua ya kuunganisha wizara na mashirika yake ya umma, kutafanya sasa Waziri, Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi na watendaji wakuu wa mashirika, kuwajibika kwa kamati moja ya PAC.
Dk Kashilillah alisema sababu nyingine ni kuangalia utendaji katika baadhi ya nchi, ambazo alisisitiza kuwa hazina kamati za mashirika ya umma.
Kutukanwa kwa Makinda, si tukio jipya kwa kuwa alipata kuzungumzia namna ambavyo amekuwa akinyanyaswa kutokana na jinsi yake na nafasi ambazo amekuwa akishika kitaifa.
Mwaka jana, wakati akifungua mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Makinda alisema alinyanyaswa baada ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo, kutokana na jinsi  yake na kuwataka Watanzania kupinga unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa dhidi ya wanawake na wasichana.
“Hata nami hadi nilipofika katika nafasi hii, nimenyanyaswa sana kutokana na jinsi yangu na hata wengine kujitokeza kusema na kuandika kupitia magazeti, hili si sawa na kila nilipokumbuka huwa naumia mno.
“Maneno huwa yanatoka hasa inapotokea mwanamke amechaguliwa au kuteuliwa kuongoza jambo fulani kwa maslahi ya Taifa, utakuta kila kona watu wanasema vibaya lakini chanzo ni jinsi yake.
“Katika hili, hata kwa mara ya kwanza nilipothubutu kujitokeza kugombea ubunge wa Njombe Kusini, wakati ule ndiyo unaingia mfumo wa vyama vingi, nilisemwa mno kutokana na jinsi yangu.
“Nilipofikia sasa najua hakuna wa kunisumbua ila kubwa tunatakiwa kila mmoja ajue wajibu wake,” alisema Spika Makinda.
Mwandishi aliwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambayo iliweka wazi kuwa hakuna sheria yoyote inayozuia mtu kutoa namba ya simu ya mwingine kwa mtu au watu wengine, bila ridhaa ya mwenye namba ya simu.
Ofisa wa TCRA, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu si msemaji wa taasisi hiyo, alisema sheria ya kuzuia utoaji namba na taarifa za mtu mwingine, inakataza kampuni za simu kufanya hivyo, lakini haizungumzi kwa mtu binafsi.
Ofisa huyo alinukuu sheria hiyo: “Taarifa ni siri ya mtu husika, isipokuwa kama mtu huyo ameitoa kwa ridhaa yake.”
Alisema pamoja na kuwapo na kipengele hicho, mtu yeyote ambaye ana namba ya simu ya mtu mwingine, hazuiwi kutoa namba hiyo kwa watu wengine.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Rashid Mtuta, alitoa kauli ya kulaani kitendo cha kuweka hadharani namba hizo za simu.
“Hivi ikitokea kesho wao wamepata uwezo wa kuongoza Dola kisha watu wakasambaza hadharani namba zao za simu watajisikiaje? Ukweli siungi mkono jambo hili na linaonesha ni namna gani viongozi hao wamekosa ustaarabu dhidi ya viongozi wenzao,” alisema Mtuta.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya   wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wamesema ingawa namba za simu za viongozi hao zinaweza zikapatikana kwa kila mtu, kuzigawa katika mkutano huo ambao ulikuwa na mtazamo hasi kwa Spika na Naibu wake,  kulikuwa na nia mbaya.
“Kama ungekuwa mkutano au semina yenye nia njema na Spika, ungesema wamegawa simu kwa nia njema. Lakini mkutano huo ulivyokuwa na kauli mbovu kwa Spika na taasisi ya Bunge, kitendo cha kuwapa watu namba kinamaanisha walitaka hao watu wamtukane pia,” alisema mmoja wa watoa maoni.
Mjumbe huyo ambaye ni mbunge hakutaka jina lake liandikwe gazetini  akisema, “katika mkutano kama huo, kunakuwa na watu wa kila aina wakiwamo wasio na busara. Hivyo viongozi hao wa Chadema waliofanya hivyo, wameshindwa kutumia busara.”
Mjumbe wa NEC, Juma Killimbah, alisema simu ya kiongozi huyo kujulikana si ajabu na ni jambo la kawaida.
“Tatizo ni maudhui. Kama kitendo hicho kina lengo zuri hakuna tatizo,” alisema Killimbah ambaye aliwahi kuwa Mbunge na kuhadharisha wananchi wasije kujikuta katika mkono wa sheria kwa kutumia namba hizo vibaya kwa kutoa matusi.

No comments: