Tuesday, February 5, 2013

SOKO LA KARIAKOO LAHAMIA NDANI YA BUNGE DODOMA...

Mkutano wa 10 wa Bunge la Jamhuri jana uliingia dosari na kuonekana sawa na fujo za sokoni Kariakoo kwa baadhi ya wabunge kuonesha dhahiri utovu wa nidhamu na uvumilivu.
Ni dhahiri kilichoonekana jana ni kitendo ambacho hakiashirii  mustakabali mwema kwa Taifa hili ambalo linawategemea wawakilishi wao hao kuwasemea na kujadili kero zao kwa njia ya busara.
Kusimama kwa wabunge na kupiga kelele kama wako sokoni kulionesha wazi kuwapo kwa mvutano wa wazi baina ya wawakilishi hao wa upinzani na wa chama tawala.
Wabunge hao wengi wao wakiwa ni wa Kambi ya Upinzani walisimama na kupiga kelele wakiomba kutoa taarifa wakati hoja ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) ikijadiliwa.
Kukosekana kwa utulivu na kuachiana nafasi ya kujadili hoja iliyokuwa mbele yao, kulifanya Bunge lionekane kama darasa la watoto watukutu wasiosimamiwa na mwalimu.
Sakata hilo lilianza pale Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliposimama kuchangia na kuzidisha muda na kumfanya Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu kutoa taarifa ya ukiukwaji huo wa kanuni na kukubaliwa na Naibu Spika Job Ndugai aliyesema Katibu alipitiwa.
Alimwongezea Profesa Maghembe dakika tatu za kumalizia mchango wake, hata hivyo alipopitiliza ndipo Mnyika na Mbunge wa Kawe Halima Mdee (Chadema) waliposimama kutaka kuhoji sababu hiyo, lakini Ndugai akawakatalia.
Ndugai aliwataka wabunge kuchangia hoja ya Profesa Maghembe aliyohusu hoja ya Mnyika kuhusu uboreshaji wa huduma za majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam, ambapo Profesa katika mapendekezo ya Serikali alitaka hoja hiyo iondolewe kwa sababu haikuwa na umuhimu wowote wakati ule kwani ilishafanyiwa kazi huko nyuma.
Alisema suala hilo lilishafanyiwa mchakato hata kabla Mnyika hajawa Mbunge wa Ubungo na hivyo hapakuwa na sababu ya kuendelea kutolewa.
Pamoja na mapendekezo hayo, Naibu Spika alimtaka Mdee awe wa kwanza kuchangia na kufuatiwa na wabunge wengine waliosimama na kuorodheshwa tayari kuchangia akiwamo Zarina Madabida (CCM), lakini baada ya Mdee kuonekana amesusa kuchangia, Madabida alipewa fursa.
Lakini alipoanza kuchangia ndipo wabunge walioonekana kuwa wa upinzani wakiongozwa na Lissu kuanza kupiga kelele za ‘taarifa! taarifa!’ Na kukataliwa na hivyo wote kuamua kusimama huku wakiendelea kugonga meza na kuimba “CCM mafisadi! CCM mafisadi!”
Hali hiyo ilipoendelea, Naibu Spika alitamka wazi kuwa hataahirisha kikao cha Bunge na kuacha Watanzania waone kilichokuwa kikifanywa na wabunge hao wengi wao wakiwa ni wa Chadema.
“Watanzania jioneeni utovu wa nidhamu unavyofanyika hapa waziwazi,” alisema Naibu Spika na kisha kunyamaza akisema waachwe waendelee kupiga kelele ndipo kikao kiendelee.
Baada ya kuonekana kukithiri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema alisimama kujaribu kuokoa hali hiyo kwa kutumia kanuni, lakini hata hivyo hakufua dafu na ndipo wabunge hao wakazidi kupiga kelele huku wakiibeza CCM.
Werema alionekana kwenda meza kuu kama hatua ya kutafuta ushauri lakini alirejea mezani kwake; hatua iliyomfanya Naibu Spika kuahirisha kikao hicho na kuomba Kamati ya Uongozi wa Bunge ikutane kujadili hali hiyo.
Hilo lilitokea baada ya Naibu Spika kuhoji wanaotaka hoja ya Mnyika iondolewe wakawazidi waliopinga na hivyo kuamua kuwa hoja hiyo imefutwa.
Baada ya kauli ya Naibu Spika, Mnyika alipiga kelele sawa na mtu anayelia huku akiungwa mkono na wabunge wengine akiwamo Lissu, Mdee  na Mchungaji Peter Msigwa na wengine ambao haikuwa rahisi kuwabaini.
Kikao cha Bunge kilipoahirishwa, baadhi wa wabunge walitoa maoni yao kuhusiana na hali ilivyokuwa ndani ya Bunge jana alasiri.
Jaji Werema alisema Bunge linaendeshwa kwa taratibu na kanuni na Mnyika alipewa nafasi akatoa hoja.
Alifafanua kwamba kwa utaratibu, zikiwapo hoja mbili; ya Serikali iliyowasilishwa na Profesa Maghembe, na ndio ilipaswa kuanza kabla ya ile ya Mnyika.
Alisema wakati malumbano yalipoanza, alisimama ili kueleza kama hoja inaleta tabu ya kuanza kujadili ya Waziri, wabunge wajadili kwa pamoja ya Mnyika na ya Maghembe na mwisho ingehitimishwa kwa Spika kuhoji wabunge na Bunge kuazimia.
Wabunge wangepewa nafasi ya kujadili ndipo ikatokea sintofahamu na kilichojitokeza ni upotevu wa muda.
“Uamuzi wa Naibu Spika ulikuwa sawa, alisema hoja ya kwanza ni ya Serikali na haiui hoja ya Mnyika ila muda wa kujadili ungekuwa mrefu,” alisema Werema.
Alisema mabunge ya vyama vingi yana desturi hizo na kinachohitajika ni uvumilivu “na sasa Kamati ya Uongozi inakaa”. Alisema “kwa mfano kuna mbunge alitoa maneno machafu wakati Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) akiondoka.

No comments: