![]() |
| James Mbatia. |
Baada
ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, kuwasilisha jana
nakala za mitaala bungeni kama alivyoahidi wiki iliyopita, hofu ya kujiuzulu
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia imegubika NCCR-Mageuzi.
Waziri
Kawambwa aliwasilisha mitaala ya elimu ya awali, msingi na sekondari ya mwaka
2005 bungeni, kabla ya kuanza kipindi cha maswali na majibu kama alivyoahidi
Januari 31.
Muda
mfupi baada ya hilo kufanyika bungeni Dodoma na Bunge kuamua kuihakiki kama
haijachakachuliwa, hofu ilitanda NCCR-Mageuzi, kutokana na kiapo cha Mbatia
kwamba ikiwasilishwa, atajiuzulu ubunge.
Kutokana
na hofu hiyo, Katibu wa Uhusiano na Uenezi Taifa, Kitengo cha Vijana wa
NCCR-Mageuzi, Deogratius Kisandu, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari
akielezea kutokubaliana na hatua ya Mbatia kujiuzulu.
Kuwasilishwa
kwa mitaala hiyo, kulitokana na hoja binafsi ya Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi akidai kwamba Serikali haina mitaala na ndiyo maana elimu nchini
inaendeshwa kwa udhaifu.
Mbatia
aliitaka Serikali iwasilishe mitaala hiyo Januari 31 na kuahidi kuwa kama
ingewasilishwa, angekuwa tayari kujiuzulu.
Kutokana
na madai hayo yaliyoendana na kiapo, Naibu Spika, Job Ndugai, alimwagiza Dk
Kawambwa kuileta mitaala hiyo bungeni jana.
Hata
hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa mitaala hiyo,
Mbatia alifanya mkutano na waandishi wa habari bungeni na kusema kwa
kuwa Serikali ilishindwa kuwasilisha mitaala Januari 31, iliyoletwa jana,
itakuwa imechakachuliwa.
Kutokana
na kauli hizo za Mbatia, baada ya Dk Kawambwa kuwasilisha mitaala hiyo kama
alivyoahidi, Ndugai aliunda Kamati ya watu sita kuichunguza kama ni halisi au
imechakachuliwa.
Naibu
Spika alisema maadam mitaala hiyo iliwasilishwa mezani kwake, jukumu la kujua
uhalisia si kazi ya mbunge, bali ya Bunge na kwa mantiki hiyo, akaunda Kamati
kuangalia uhalisia wake.
Alitaja
wajumbe sita wa Kamati hiyo kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii za
Bunge, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, Margaret Sitta (CCM) na Mbunge wa
Kibiti, Abdul Marombwa (CCM).
Wengine
ni Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassim Yahya (CCM); Mbunge wa Viti Maalumu,
Bernadetha Mshashu (CCM); Mbunge wa Karatu, Israel Natse (Chadema) na Mbunge wa
Gando, Khalif Suleiman Khalifa (CUF).
Pamoja
na kuunda Kamati, Naibu Spika alimruhusu
Mbatia kushirikiana na Kamati hiyo pamoja na watendaji kutoka
serikalini, ili kuhakiki mitaala kama imechakachuliwa au la.
Alisema
kama Kamati hiyo itabaini mitaala ni halisi, wataigawa kwa wabunge kwa ajili ya
matumizi yao.
Pamoja
na kuwa Mbatia hajazungumzia kujiuzulu kwake, wala Bunge halijamtaka achukue
hatua kutekeleza kiapo hicho, Kisandu katika taarifa yake alisema:
“Sisi
vijana wa NCCR-Mageuzi tunasema hatutakubali Mwenyekiti wetu ajiuzulu ubunge,
eti kwa sababu mitaala imepatikana, kwani Serikali ilikuwa wapi kuitoa tangu
miaka yote hiyo mpaka Mbatia ‘akakomalia’ ndipo ipatikane?
“Hajiuzulu
mtu hapo, kwa nini hawakupeleka siku ile aliyotaka Mbatia? Je, kama wamekwenda
kuitengeneza, kuna uhalali gani wa Mbatia kujiuzulu? Tuamke Watanzania,”
alieleza Kisandu.
Alisisitiza
kuwa kama Serikali ingepeleka mitaala siku ambayo Mbatia aliiomba,
wangekubaliana naye ajiuzulu, lakini kwa kuwa muda umepita, hawakubali
ajiuzulu.
“Hakuna
haja ya kujiuzulu. Waulize walimu na wakufunzi wao na maprofesa wao kama
wamewahi kuiona pamoja na kuwa na kozi inayohusu mitaala vyuoni, hebu nenda shuleni
na vyuoni kama utaiona.
“Sasa
Mbatia kafungua ukurasa mpya, shinikizo lake limewezesha hata wadau waone
mitaala ya elimu ya Tanzania. Rai yangu magazeti yaichapishe ili nasi tufaidi
yaliyomo,” alishauri.

No comments:
Post a Comment